Makala

CHOCHEO: Siache corona kupangua harusi

May 30th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

DERRICK na Eva walikuwa wamekamilisha mipango yote ya harusi yao kabla ya janga la corona kuvamia ghafla.

Walikuwa wamealika watu 500 wakiwa ni jamaa na marafiki wa mbali na karibu. Aidha walipanga kusafiri hadi Mauritius kwa fungate kabla ya kurejea nchini kuendelea na maisha ya ndoa.

Hata hivyo, mipango yote ilisambaratishwa na janga hili na wakalazimika kufunga harusi bila mbwembwe walizotarajia.

“Hatukuweza kuahirisha harusi kwa sababu tungepata hasara zaidi, sio ya kiasi cha pesa tulichotumia kuipanga bali hasara ya hisia zetu. Tulikuwa tumepanga kuanzisha familia na kuahirisha harusi ingekuwa sawa na kuahirisha hatua muhimu katika maisha yetu. Tuliamua kula kiapo mbele ya padre, wasimamizi na wazazi wetu pekee na tumesonga mbele na maisha huku tukijilinda na corona,” asema Eva.

Mwanadada huyu asema kwamba alikuwa amechumbiana na Derrick kwa miaka minne na hakuna chochote kingemzuia kuwa mke wake tarehe waliokuwa wamepanga.

“Corona haingebadilisha mipango yetu baada ya kujuana kwa miaka minne. Tumetimiza ndoto yetu kwa sababu ya upendo wetu na kwa kuuheshimu kwa dhati. Ndoa ni ya wawili na wengine ni mashabiki tu. Kukosa kwa wageni na mabusu hadharani hakufai kuwa kisiki katika ndoa wakati huu wa janga la corona,” asema Eva.

Kulingana na Derrick, ilibidi wafutilie mbali safari yao kwenda fungate baada ya safari za ndege kusitishwa na hata anakiri kuwa walitafuta ushauri wa wataalamu baada ya marufuku hiyo ya serikali.

“Kusema kweli, binafsi niliathirika sana serikali ilipofunga makanisa lakini mchumba wangu alinishawishi tumuone mshauri nasaha. Tuliamua kuwa harusi itaendelea kwa kuzingatia kanuni za serikali,” anasema Derrick.

Kulingana na wataalamu, mbwembwe zinazoshuhudiwa wakati wa harusi sio sehemu ya ndoa mbali ni nakshi kama mapambo mengine.

“Sio vibaya harusi kuwa na mbwembwe kwa kuhudhuriwa na walioalikwa na wasioalikwa. Hata hivyo, ndoa halisi ni maharusi kulishana viapo, kuwepo kwa mashahidi wanaotia sahihi cheti cha ndoa na harusi kufuata utaratibu wa kisheria kikamilifu,” asema mshauri wa ndoa Jeniffer Karimi wa kituo cha Maisha Mema, jijini Nairobi.

Karimi asema kanuni za kuzuia kusambaa kwa corona hazifai kuzuia watu kufunga harusi.

“Inachukua muda, nguvu na rasilmali kupanga harusi na janga la corona halikutarajiwa. Kwa hivyo, wachumba wanafaa kuzungumza na wakielewana, wafunge harusi yao kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa. Ndoa ni ya wawili, wanaohudhuria hawaishiriki,” asema na kuongeza kuwa hali ya sasa imepunguza gharama ya harusi.

“Huwa nawaliwaza wanaosononeka baada ya mipango yao ya harusi kuvurugwa na corona kwa kuwaambia ni afueni kwao nyakati hizi ngumu kiuchumi. Huwa nawakumbusha kuwa watu waliokuwa wamealika wangewaachia hasara tu,” asema Karimi.

Kulingana na Daniel Kisesi, mshauri wa wanandoa katika shirika la Grace for life, mjini Machakos, uamuzi wa kuahirisha harusi unafaa kuwa wa wachumba wote wawili.

“Corona imevuruga ndoto za watu wengi waliotamani kuwa na harusi ya kufana na fungate ya kukumbuka. Kanuni za kuzuia janga hili ziliwaacha na chaguo mbili, kuahirisha harusi au kuzifanya faraghani. Uamuzi wa kuahirisha harusi unahitaji kuafikiwa na wachumba wote wawili,” asema Bw Kisesi.

Anasema kwamba watu wanafaa kubadilika jinsi nyakati zinavyobadilika.

“Kuna uwezekano kwamba hali iliyosababishwa na corona itaathiri mitindo ya maisha kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na sherehe za harusi na kwa hivyo ushauri wangu kwa watu ni kukumbatia mabadiliko hayo na kula yamini badala ya kuahirisha awamu hii muhimu katika maisha yao,” asema.