Makala

CHOCHEO: Ufanyeje akilisaliti penzi lenu?

March 23rd, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

SI siri kwamba wengi waliosalitiwa na wapenzi huchelea na hata kuchukia mapenzi.

Hasa, huwa hawataki kuwaona waliowasaliti na baadhi huamua kutopenda tena katika maisha yao.

Hali huwa mbaya zaidi endapo unaishi nyumba moja na kulala kitanda kimoja na aliyekusaliti kimapenzi.

“Inauma kujua kwamba aliyelala kando yako aligawa pembeni licha ya kumpa moyo na mwili wako wote. Inakeketa maini hata zaidi kuishi nyumba moja na msaliti licha ya wewe kumpenda, kumuamini kwa dhati. Hilo husababishia mtu masononeko makubwa,” asema mwanasaikolojia Derrick Owuor wa kituo cha Love Care jijini Nairobi.

Anasema kwamba baada ya kusalitiwa, mtu huingiwa na hisia za chuki ambazo huwa ni vigumu kuzifuta.

“Kuna wale wanaonyamaza wakijua kwamba wachumba wao huwasaliti na mipango ya kando. Kuna wanaoamua kulipiza kisasi kwa kutafuta wachumba wa nje au kuwakabili wapenzi wao,” asema Bw Owuor.

Anaongeza kuwa kunyamaza kunaumiza zaidi kwa sababu hakusuluhishi chochote.

“Mtu akinyamaza na kuugulika ndani, huwa anajizidishia maumivu moyoni. Anaweza kupata matatizo ya kiafya na kiakili. Na akilipiza kisasi, huwa kuna hatari kubwa kwa sababu huwezi ukasuluhisha makosa kwa kufanya makosa,” aeleza mwanasaikolojia huyu.

“La muhimu kufanya ni kuhakikisha mpenzi anajua kwamba unafahamu anacheza nje, iwe ni kwa kumpata peupe au umetumia njia tofauti kuthibitisha hayo. Hata hivyo, ni muhimu kuepuka ugomvi unaoweza kuzua hatari kwa maisha yako,” asema.

Mwambie ajue

Kufungua moyo na kueleza mtu kwamba unajua anakusaliti kimapenzi na una ushahidi anacheza nje, kunasaidia kuepuka msongo wa mawazo unaosababisha matatizo ya kiakili na kimwili. Wataalamu wanasema mtu akiomba msamaha na asirudie, huwa anaimarisha uhusiano wa kimapenzi.

Kulingana na wataalamu, kuna wanaochovya nje kwa sababu ya wenzao kutowaridhisha chumbani.

“Hii ndio sababu mawasiliano mazuri ni muhimu katika mapenzi ili kila mmoja amwage hisia zake kuhusu jambo linalowatatiza na kusuuza roho pia. Mawasiliano husaidia sana kuboresha huduma kwa mwenzio,” asema Frida Epo wa shirika la Big Heart Nairobi.

Mtaalamu huyu anasema usaliti wa mapenzi ni hatari sana.

“Unaweza kusababisha mauti, hasa ikiwa mtu amewekeza hisia, mali na wakati wake kwa msaliti. Badala ya kusaliti mtu, zungumza naye, mnaweza hata kuachana ingawa sio wengi wanaoweza kukubali kutamatisha uhusiano kwa kimapenzi roho safi,” asema.

Bi Epo anasema ni heri kuachana na mpenzi anayekusaliti mara kwa mara kuliko kusononeka ukiishi na kulala naye kitanda kimoja.

“Ushauri wangu ni kwamba anayekusaliti kisha arudie, hana mapenzi ya dhati. Hivyo basi, badala ya kuendelea kusononeka, ni heri kumuacha na kuepuka hatari,” asema.

Kwa wanaoshuku kuwa wachumba wao huwa wanawasaliti, wataalamu wanashauri wafanye uchunguzi wa kina kwanza ili kubaini ukweli.

“Wakati mwingine watu huongozwa na wivu na kudhani wapenzi wao wanawasaliti. Ni muhimu kufanya uchunguzi kwanza kabla ya kumkabili mtu au kuchukua hatua na hauna ushahidi wa kutosha,” aeleza Bi Epo.

Kulingana na wataalamu, mtu anayekusaliti kimapenzi hakuheshimu kamwe.

“Ni vigumu kwa watu wanaoheshimu wapenzi wao kuwasaliti. Penzi likijengwa kwa misingi ya heshima, huwa linanawiri,” aeleza Bw Owuor.

Anashauri watu kutafuta huduma za wataalamu au viongozi wa kidini wanaoheshimika, misukosuko inapozuka.

“Kuna watu wanaogawa uroda kwa sababu ya tamaa za kimwili na mali na hilo ni hatari zaidi kwao na kwa uhusiano wao,” aeleza mtaalamu huyu.