Makala

CHOCHEO: Ufanyeje akipoteza figa?

November 21st, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

“PAT hanitaki siku hizi. Anasema mimi sio yule demu alioa miaka mitano iliyopita nilipokuwa na figa 8. Tatizo lake ni kuwa nimekuwa mnene baada ya kujifungua na sio kupenda kwangu,” Karimi mwanadada mwenye umri wa miaka 29, alalamika.

Mwanadada huyu anasema kwamba anahofia huenda mumewe akaanza kuhanya na vipusa wenye umbo analotamani. Cha kushangaza ni kuwa si Karimi peke anapitia hayo.

Mary, mwanadada mwenye umri wa miaka 33 anajichukia baada ya mumewe kulalamika kuwa sura na umbo lake zimebadilika tangu harusi yao miaka tisa iliyopita.

“Anasema ninafaa kudumisha sura na umbo langu, nibaki yule kidosho aliyefunga pingu za maisha naye ingawa sasa mimi ni mama wa watoto wawili,” asema Mary.

Kulingana na mwanadada huyu, hii imefanya uhusiano wake na mumewe kuingia doa.

Wataalamu wa masuala ya ndoa na lishe bora wanasema kwamba ingawa ni muhimu kudumisha umbo zuri, mtu hubadilika miaka inaposonga hasa wanawake wakiolewa na kujifungua.

“Wanaume wanafaa kuelewa kuwa sura na umbo la mwanamke hubadilika miaka inaposonga sanasana wanapojifungua. Kuna wale wanaorudia umbo lao la awali na kuna wale ambao hairudi hata wakijaribu lishe na mazoezi,” asema Rukia Hirsi, mtaalamu wa lishe na afya ya wanawake katika shirika la Mirage, jijini Nairobi.

“Kuna homoni za mwili wa mwanamke zinazosababisha mabadiliko umri unaposonga, anapopata watoto na hata anapokuwa kwenye ndoa isiyo na misukosuko. Kuridhika tu kunaweza kufanya mwanamke kuongeza uzani wa mwili na kupoteza umbo na sura aliyokuwa nayo kabla ya kuolewa,” asema Rukia.

Mtaalamu huyu anasema kuwa wanawake wanaweza kudumisha umbo lao kwa kuepuka vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi na kufanya mazoezi.

“Usile kila kitu. Hakikisha unaepuka mapochopocho na upate chakula bora kisicho na mafuta mengi. Fanya mazoezi ambayo pia ni muhimu kwa afya yako,” asema.

Wataalamu wanasema badala ya kuwalaumu wake zao, wanaume wanafaa kuwasaidia kudumisha saizi ya mwili wanayopenda.

Lalama

“Kubadilika kwa umbo la mwili hakufai kuwa tisho kwa ndoa. Wanaume wanafaa kusaidia wachumba wao badala ya kuwalaumu na kutumia hicho kama kisingizio cha kuchepuka. Hata wanaume huwa wanajipata katika hali hii umri unaposonga, wakioa na wasipofanya mazoezi,” asema Godfrey Kyule, mshauri wa wanandoa wa shirika la Amani Purpose, mtaani Kitisuru, Nairobi.

Jairus Sumba, mwanamume mwenye umri wa miaka 31, alijipata katika hali hii miaka mitatu baada ya kuoa.

“Sijui nyama za mwili zilitoka wapi. Niliongeza uzani kutoka kilo 66 hadi 102 na mke wangu akaanza kulalamika kwamba nimekuwa mzembe chumbani. Tulijadili suala hilo na baada ya kupata ushauri kuhusu lishe na mazoezi, huwa ninachezea kilo 78 na 81,” asema Sumba.

Anasema kuwa mabadiliko katika mwili wake yalitokana na amani ambayo mkewe alimpatia baada ya harusi.

“Akili yangu ilitulia baada ya kuoa. Mke wangu hakunipa ‘stress’ hata kidogo,” asema.

Jayreen Chomba, mama ya watoto watatu anasema kwamba amedumisha umbo lake kwa kuzingatia lishe na mazoezi.

“Sijawahi kuwa na zaidi ya kilo 60 bila mimba. Hata baada ya kujifungua, huwa ninahakikisha ninapata lishe bora. Nashauri wanawake kutotafuna na kuchangamkia vyakula vya hotelini ikiwa wanataka kudumisha umbo bora,” asema.

Rukia anasisitiza kuwa wanaume hawafai kulaumu wake zao kwa mabadiliko ya umbo mbali wanafaa kuwasaidia.

“Mili ya wanawake ni tofauti na ya wanaume. Ikiwa unampenda mtu wako, elewa mabadiliko ya mwili wake na umsaidie badala ya kumlaumu,” asema.

“Sisemi wanawake wajiachilie lakini mara nyingi wanaume huwa wanachangia mabadiliko ya mili ya wake zao,” asema.