Makala

CHOCHEO: Ukarimu wake ni chambo tu!

February 1st, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KWA kipindi cha miezi tisa, Betty alimchukulia Dan kuwa rafiki yake wa dhati.

Dan alimsaidia kwa mambo mengi kikazi na alimheshimu sana.

Dan alifahamu mumewe na marafiki zake wengi. Mwanadada huyu alihisi salama akiwa na Dan na hakufikiria kwamba mtu aliyemheshimu alikuwa na nia fiche katika moyo wake hadi majuzi.

“Nilishtuka aliponiambia kwamba ananipenda na kuomba nimlishe tunda,” afichua Betty.

Dan alimweleza kwamba alikuwa akimfanyia wema wote kwa sababu alikuwa akimpenda.

“Aliniambia alishindwa kuvumilia na akaamua kufungua moyo wake kwangu. Nilikataa kumeza chambo na tangu siku hiyo amenichukia na hanisalimii kamwe,” aeleza Betty.

Wataalamu wanasema kwamba kuna wanawake wengi wanaojipata katika hali aliyojipata mwanadada huyu.

“Wanaume wengi huwa ni fisi wanaovalia ngozi ya kondoo. Wanakuwa wakarimu kwa wanawake, wanawasaidia wakijifanya marafiki wa kawaida ilhali ndani wanasitiri hisia za mapenzi huku wakisubiri wakati wa kuwapasulia yaliyo katika mioyo yao,” aeleza Sammy Kariuki, mtaalamu katika shirika la Love Care, jijini Nairobi.

Anasema wanaume kama hao huwa wanawatendea mema wanawake wanaowalenga ili kuutumia kama chambo cha kuwanasa. “Wanajifanya marafiki wa kawaida na baada ya wanawake hao kuwaaamini, wanawafungulia mioyo yao. Kuna wanawake wanaoangukia mitego ya wanaume hawa na kuna wanaokataa kama Betty na kulinda heshima yao,” aeleza Kariuki.

Wataalamu wanasema wanaume kama hao hutumia muda kuelewa udhaifu wa wanawake hao ikiwa ni pamoja na matatizo wanayopitia katika ndoa zao au uhusiano wao wa kimapenzi. “Baadhi ya wanawake huwafungulia wanaume milango ya kutaka kushiriki ufuska nao kwa kuwasimulia matatizo wanayopitia katika ndoa zao au kujadili mahusiano yao. Kufanya hivi kunafanya mwanamume kama huyo kuwa na hisia za kutaka kujaza pengo lililopo katika maisha ya mapenzi ya mwanamke husika,” aeleza Jane Wausi wa shirika la Big Hearts, jijini Nairobi.

Anashauri wanawake kutochukulia wanaume wanaowatendea mema kama malaika. “Wema wowote, ukarimu wowote anaokuonyesha au kukutendea mwanamume asiye mumeo au mpenzi wako kwa muda mrefu, huwa sio wa kawaida. Huwa kuna njama fiche na usipokuwa mwangalifu ni rahisi kujipata ukishiriki ufuska,” aeleza Wausi.

Anasema pia kuna wanawake wanaotumia mbinu hii kuwanasa wanaume.

“Pia kuna wanawake wanaojifanya marafiki na wanaume wakiwa na nia ya kuwanasa kimapenzi. Wakikosa kufanikiwa, wanawachukia wanaume hao,” aeleza.

Kariuki anasema ni kawaida ya watu wanaohusiana kwa muda mrefu wakiwa marafiki kuanza kumezeana mate hasa ikiwa hakuna siri kati yao.

“Huwa inaanza watu wanaposimuliana wanayopitia katika maisha yao ya mapenzi. Kwa mfano mwanamke akimweleza rafiki yake mwanamume kuhusu mapungufu ya mumewe katika tendo la ndoa au mwanamume akimweleza mwanamke kuhusu tabia za mkewe,” asema.

Kulingana na Mhubiri Joseph Mugambi wa kanisa la Hope in Christ, jijini Nairobi, urafiki kati ya wanaume na wanawake walio katika ndoa unafaa kuwa na mipaka.

“Ni rahisi mtu kumtumbukiza rafiki katika majaribu akimsimulia kuhusu matatizo ya ndoa au mahusiano ya mapenzi. Hii ndiyo sababu unapata watu wakizini na wake au waume wa marafiki zao,” aeleza.

Anashauri watu kutafuta huduma za washauri waliohitimu wanapopata matatizo katika ndoa zao.

Wausi anakubaliana na Mhubiri Mugambi kuwa kuna haja ya watu kuweka mipaka wanapopiga gumzo na marafiki.

“Unafaa kupima kwa uangalifu kila tendo la wema unalofanyiwa na rafiki mwanamume au mwanamke ili asiwe analenga kukutumbukiza katika ufuska,” ashauri.