Makala

CHOCHEO: Usiende deti ukiwa mlevi, pombe ni adui wa penzi la dhati

November 30th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

SALLY alipompigia simu James kuthibitisha deti yao ya kwanza, barobaro huyo hakuamini ilikuwa kweli.

Alikuwa amemrushia kipusa huyo mistari kwa miaka mingi lakini alichogundua siku hiyo ni kwamba hakuwa na ujasiri wa kumfungulia moyo wake kumweleza alivyompenda.

James alipitia katika baa iliyokuwa karibu na kubugia chupa kadhaa za bia ili kupata ujasiri wa kumwaga moyo wake kwa Sally.

“Ninajutia kitendo hicho. Japo Sally alivumilia kwa masaa manne akinisikiliza, ujumbe alionitumia baada ya deti yetu ulikuwa wa kutamausha. Alinikataa kwa sababu ya ulevi wangu ilhali ilikuwa mara yangu ya kwanza kunywa pombe na nilifanya hivyo kupata ujasiri wa kumuingiza boksi,” asema James.

Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema ni makosa kwa mtu anayetafuta mpenzi wa kudumu kulewa wakati wa deti ya kwanza.

“Ikiwa unakutana na mtu unayetaka awe mchumba wako, basi epuka pombe siku ya kwanza. Kufika katika miadi ukiwa mlevi kunaonyesha kuwa haujiamini. Vipusa hutaka wanaume wanaojiamini na sio wanaotumia vileo kupata ujasiri wa kuwatongoza,” aeleza Bi Benta Asiyo, mwanasaikolojia katika kituo cha Afya Love jijini Nairobi.

Anasema wanawake waadilifu wanaotafuta mapenzi ya dhati huamini kuwa mtu akiwarushia chambo akiwa mlevi huwa anaficha tabia zake halisi.

“Kwa kawaida watu wanapolewa, huwa hawamaanishi wanachosema na hata kujielewa vizuri. Hivyo basi, mwanamke anayetafuta mpenzi wa dhati huchukulia maneno ya mwanamume mlevi kama mzaha tu,” aeleza Bi Asiyo.

Mtaalamu huyu anaongeza kuwa mtu anayekutana na mpenzi kwa mara ya kwanza akiwa mlevi anaweza kukosea heshima iwe kwa tabia au matamshi.

“Akina dada wengi huwa wanatafuta kitu spesheli kwa mtu kabla ya kukubali kuanza uhusiano wa kimapenzi. Tafiti zimeonyesha kuwa hakuna kitu spesheli kwa mtu mlevi kwa sababu tabia ya walevi wote ni sawa,” aeleza.

Kevin Nahai, mwanasaikolojia katika shirika Soul Mate anasema mtu akiwa mlevi hawezi kufanya maamuzi mema, hajitambui na hawezi hata kumfahamu vyema anayenuia kuwa mpenzi wake.

“Kukosa kulewa siku ya kwanza ya kujivinjari na mpenzi wako, kunakupatia fursa ya kumdadisi vyema na kuelewa tabia zake na kukuelewa pia,” aeleza Nahai.

Anasema kuepuka pombe katika mkutano wa kwanza na mtu unayemrushia chambo kunasaidia kung’amua iwapo uhusiano wako naye unaweza kunawiri.

“Mtu anapolewa akiwa na mtu anayemmezea mtu, anaweza kujidaganya kuna mapenzi kati yao hadi pale pombe inapomtoka anapogundua alijikosea mwenyewe,” aeleza.

Majuto

Kulingana na Bi Asiyo, watu wengi huwa wanajuta kwa maamuzi wanayofanya kwa sababu ya kulewa wanapokutana kujivinjari siku ya kwanza.

“Kuna wale wanaojipata wamelishana uroda na kujutia kitendo hicho hasa wote wakilewa. Mtu mlevi hawezi kufanya maamuzi ya busara. Usishawishiwe kulewa na mtu mnayekutana mara ya kwanza kwenye deti, utajuta,” asema.

Wataalamu wanashauri vipusa kuwaepuka wanaume wanaowaalika kujivinjari kwenye baa wakisema kuna hatari baada kulewa.

“Kuna maeneo mengi ya kuvutia mnayoweza kukutana kuzungumzia mambo yenu. Jiulize, kwa nini anataka tukutane eneo la burudani mara ya kwanza iwapo anataka kweli niwe mchumba wake wa dhati,” aeleza Nahai.

“Ukiona mwanamume anayekurushia mistari akikualika kilabuni kwa mkutano wenu wa kwanza, huyo hataki mpenzi wa dhati mbali ni kupitisha wakati tu. Mapenzi ya dhati hayapaliliwi katika ulevi,” asema.

Badala ya kubugia pombe kupata ujasiri wa kufungulia kipusa moyo wako, wataalamu wanashauri wanaume kujipeleleza kwanza.

“Uhusiano wa kwanza wa kimapenzi huwa unaanza na mtu binafsi. Tafuta njia za kujipenda kwanza na ulimwengu utakupenda na bila shaka sio kwa sababu ya ulevi. Ulevi unafanya mbegu za mapenzi kukosa kuota na zikiota hazinawiri na zikinawiri, hukauka kabla ya kukomaa,” asema Nahai.