Habari Mseto

Chokoraa waelezea hofu yao kaunti ikianza kuwasajili

June 18th, 2019 2 min read

NA RICHARD MAOSI

Vijana wa kurandaranda mitaani ya Nakuru wameelezea hofu yao baada ya serikali kuanzisha shughuli ya kuwasajili ili kupata idadi yao kamili.

Wakizungumza na Taifa Leo Dijitali, baadhi yao wanasema kaunti ina njama fiche ya kuwaangamiza, kwani hawana makazi mengine watakayoita nyumbani.

Wengi wao wanategemea vibarua ama ambaomba,ili kukidhi mahitaji yao ya kila siku ikiaminika kuwa baadhi yao walizaliwa barabarani na hawajui asili yao.

Kupitia msemaji wao Alfred Kibet (sio jina halisi), anaona afadhali wangetafutiwa njia mbadala ya kujitegemea badala ya kuhangaishwa.

Vijana wa mitaani kutoka kaunti ya Nakuru wakijiandaa kuoga,baada ya kujitengenezea bafu. Picha/ Richard Maosi

Mara nyingi wamekuwa mbioni kutafuta hifadhi polisi wanapoendesha msako mkali,katika harakati ya kuzima magenge hatari mjini.

Siku za hivi karibuni madai yamekuwa yakizuka kuwa chokoraa wamekuwa wakishirikiana na wahalifu kutoka mitaa ya Kivumbini, Bondeni na Rhonda kuhangaisha raia, dai ambalo limepingwa vikali na Alfred Kibet akisema huo ni uongo mtupu.

Kibet alisema wahuni wanaoishi mitaani ndio wamekuwa wakitorokea mjini Nakuru kutafuta maficho, ili wasinaswe na polisi.

Chokoraa katika barabara ya Kenyatta Avenue, mjini Nakuru. Picha/ John Njoroge

Alieleza jinsi wengi wao wamekuwa wakijifanya ni chokoraa na wamekuwa wakiharibia jina jumuia ya vijana wanaorandaranda.

“Kwa kweli hatuwezi kusema kuwa ni wote lakini idadi kubwa ya machokoraa, walikimbia makwao kutokana na changamoto za kimaisha,” alisema.

Alieleza kuwa lanbda ni njia ya kuwatupa wengine wao msituni Baringo kama ilivyo fanyika mapema Februari mwaka huu.

“Wakati wa msako wengine wetu wasiokuwa na hatia wamekuwa wakiingia kizuizini bila kufanya makosa yoyote,” akasema.

Ann Wanjiru 14 amekuwa akiishi barabarani kwa miezi miwili sasa,tangu maisha ya kukaa na baba mzazi yashindikane.

Chokoraa wakipokea ushauri katika hospitali ya Nakuru Level 5 kila siku ya jumatano. Picha/ Richard Maosi

Alisema alilazimika kuacha shule akiwa katika kidato cha pili na akatoroka nyumbani mateso yalipozidi.

Ann anasema alikuwa akisomea katika shule ya upili eneo la Marugoine Lanet na kufikia sasa akipata mfadhili angerejea shuleni kukamilisha masomo yake.

“Ninatamani kurudi shule niendelee na masomo isipokuwa sina mtu wa kunilipia karo,”alisema.

Aliongezea kuwa baba yake alikuwa ni mraibu wa kuvuta bangi na hawangesikizana,hivyo basi ni afadhali aendelee kuzurura.

Hii ni baada ya serikali ya Nakuru kupitia gavana Lee Kinyanjui kutangaza wiki iliyopita kuwa, serikali ilikuwa na mradi wa kuanzisha data ya kuwasajili.

Dkt Oloo kutoka Nakuru akiwazungumzia vijana wa mtaa katika hamasisho linaloandaliwa kila wiki. Picha/Richard Maosi

Lee alisema kuwa hili lingesaidia familia ambazo hazina makazi maalum ila zinaishi katika barabara.

Aidha kaunti ya Nakuru imekuwa ikishuhudia visa vya ongezeko la idadi ya vijana wanaorandaranda mitaani, wengi wao wakitokea kaunti jirani za Baringo,Uasin Gishu na Nairobi.

Alieleza kuwa baada ya kipindi cha wiki mbili asilimia kubwa ya vijana watakuwa wamesajiliwa na hili litasaidia kuwarejesha wengine wao nyambani.