Christian Eriksen akubali kujiunga na Man-United baada ya mkataba wake na Brentford kutamatika

Christian Eriksen akubali kujiunga na Man-United baada ya mkataba wake na Brentford kutamatika

Na MASHIRIKA

KIUNGO mzoefu wa timu ya taifa ya Denmark, Christian Eriksen, 30, amekubali kujiunga na Manchester United bila ada yoyote.

Hii ni baada ya mkataba wake wa muda mfupi na Brentford inayonolewa na kocha Thomas Frank kutamatika rasmi mwishoni mwa Juni 2022.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, Man-United wamekubali pia kumpokeza Eriksen mkataba wa miaka mitatu ugani Old Traffford.

Eriksen ambaye pia amewahi kuchezea Barcelona na Inter Milan, anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa na kocha Erik ten Hag baada ya beki Tyrell Malacia kushawishiwa na Man-United kuagana na Feyenoord ya Uholanzi.

Eriksen alikatiza uhusiano wake na Inter baada ya kuwekewa kifaa cha Implantable Cardioverter Defibrillator (ICD) kumsaidia kupumua baada ya kupata matatizo ya moyo wakati wa mechi iliyowakutanisha na Finland kwenye fainali za Euro 2020. Wachezaji walio na vifaa vya ICD hawakubaliwi kuchezea kikosi cha Serie A.

Spurs waliowahi kujivunia huduma za Eriksen kati ya 2013 na 2020 hawakuonyesha nia ya kutaka tena kumsajili kiungo huyo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kocha Duncan Ferguson aagana na Everton ili ajikuze zaidi...

Barcelona yasajili vigogo Franck Kessie na Andreas...

T L