Habari za Kitaifa

Christine Kilalo alaani visa vya mauaji ya wanawake

January 31st, 2024 2 min read

NA LUCY MKANYIKA

NAIBU Gavana wa Kaunti ya Taita Taveta, Bi Christine Kilalo, ameungana na viongozi wengine kulaani vikali visa vya mauaji ya wasichana na wanawake vinavyoendelea kuripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja na wakazi kupitia ukurasa wake rasmi wa Facebook, Bi Kilalo alisema kuwa hakuna mwanamke anayestahili kudhulumiwa au kuuawa kwa sababu yoyote ile na kwamba maisha ya wanawake ni ya thamani kubwa.

“Si sawa watu kuuana. Kwa sasa tunapitia changamoto nyingi za maisha ambazo ni pamoja na mfumkobei. Tunafaa kuishi kwa amani na si wakati wa kupigana na kuuana ila kutafuta suluhu ya kusaidiana kukabiliana na shida hizi,” alisema Bi Kilalo.

Bi Kilalo aliwataka wanaume kuchukua jukumu la kulinda maisha ya wanawake na wasichana na kulaani visa hivyo vya mauaji.

Alisema kuwa wanaume wanapaswa kuwa walinzi na si wauaji wa wanawake.

“Ninatoa wito kwa wanaume wote wenye nia njema kuungana na sisi katika kupinga mauaji haya ya kinyama. Wanawake ni mama zetu, dada zetu, wake zetu na binti zetu. Wanastahili heshima, upendo na usalama. Wanaume, tafadhali, simameni na wanawake wetu,” alisema.

Hata hivyo, Bi Kilalo alikiri kuwa kuna baadhi ya wanaume na vijana wanaopitia dhuluma za kijinsia lakini alisema kuwa wanawake na watoto ndio huathirika sana.

“Si haki mwanamume au mwanamke kudhulumiwa. Lakini, kunapokuwa na changamoto za kijamii wanaoumia sana ni wanawake na watoto. Kinachosikitisha sana ni kuwa baadhi ya kesi hizi husababisha vifo,” alisema.

Vilevile, Naibu Gavana huyo aliwataka wasichana wa umri mdogo kuwa waangalifu wanapokutana na watu wasiowajua katika sehemu zisizo za umma.

Aliwashauri kuwa na subira katika maisha na kutafuta njia halali za kujikimu.

“Tunajua hali ya maisha imekuwa ngumu lakini nakushaurini wasichana kujilinda na kuepuka kukutana na watu msiowafahamu kabla ya kujuana nao vizuri,” akasema.

“Ukipanda mti huwezi pata matunda wakati huo. Mpaka uutunze ndio utoe matunda na ndivyo hivyo maisha yalivyo. Mpaka tuwe na subira na maadili ili tufaulu. Msihatarishe maisha yenu,” akaendelea kusema.