Chui, Blades mabingwa Hoki ya taji la Easter

Chui, Blades mabingwa Hoki ya taji la Easter

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Chui A na Blades B kila moja imetawazwa mabingwa kwenye mechi za taji la KHU Easter, katika magongo ya wanaume na wanawake mtawalia zilizochezewa ugani City Park, Nairobi.

Midume wa Chui waliojumuisha wachezaji wa timu ya taifa walitawazwa mabingwa walipozaba Kenya Police mabao 2-0 katika fainali. Chui ilipata ushindi huo kupitia juhudi za Allan Iningo na George Mutira waliotikisa wavu mara moja kila mmoja.

Nao warembo wa Blade B walinyuka Mombasa Sports Club (MSC) mabao 2-1 kupitia mipigo ya mikwaju ya penalti baada ya kutoka sare tasa. ”Shindano hilo lilionyesha wazi wachezaji wengi wanazidi kuboresha mchezo wao,” mshirikishi wa shindano hilo, Peter Mwathe alisema.

Naye kocha wa Kenya Police, Patrick Mugambi alisema ”Bado nikitazama mchezo wa kikosi changu haupo sawa tulipaswa kubeba taji hilo sina shaka kutaja kuwa bado vijana wangu wanapaswa kukaza buti.”

Kwenye nusu fainali ya wanaume, Chui A ilikomoa Chui B kwa mabao 3-1. Naye David Sibweche alitikisa wavu mara moja na kubeba Kenya Police kuzoa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wazalendo.

Kitengo cha wanawake, Margaret Karimi alicheka na wavu mara moja na kusaidia MSC kufunga Rising Blades bao 1-0 nayo Blades B ilizoa ushindi wa mabao 1-0 dhidi ya Blades A.

You can share this post!

Mwaniaji MCA azua ucheshi akidai 2017 alinyimwa fursa...

Zetech yazidi kuwika kwenye karate

T L