Habari Mseto

Chui mweusi adimu apatikana Kenya

February 13th, 2019 1 min read

MASHIRIKA na CHARLES WASONGA

IMEBAINIKA kuwa chui mweusi adimu kupatikana angalipo duniani. Wataalamu wametoa video ya mnyama huyo akitembea nchini Kenya, mara ya kwanza kwa picha ya mnyama huyo kunaswa barani Afrika tangu mwaka wa 1909.

Nich Pilfold ambaye ni mtaalamu wa wanyamapori anayehudumu katika hifadhi ya wanyama kule San Diego alisema ilikuwa ni bahati kwao kunasa video hiyo.

Pilfold na wenzake walikuwa wameweka kamera maalum kufuatilia idadi ya chui karibu na hifadhi ya wanyama ya Loisaba katika kaunti ya Laikipia 2018. Hii ni baada ya wao kupata habari ambazo hazikuthibitishwa kwamba kuna uwezekano wa chui huyo kuonekana.

“Tuliweka kamera zetu katika maeneo ambako ilisemekana kuwa chui alionekana,” Pilfold akasema Jumanne jioni. “Baada ya miezi michache tuliweza kuona picha kwenye kamera zetu,”

Chui huyo wa kike ana ngozi nyeusi kutokana na chembechembe za melanine ambayo huzalisha kiwango kikubwa cha rangi hiyo, Pilfold akasema

Habari za kuonekana kwa chui huyo mweusi zilichapishwa katika jarida la “African Journal of Ecology”

Chui huchukuliwa kama wanyama wanaokabiliwa na hatari ya kuangamia kulingana na ukadiriaji uliofanywa shirika la International Union for Conservation of Nature’s Red List of Threatened Species.

Hata hivyo, kiwango kamili cha kupungua kwa idadi ya wanyama hao hakijabainika, hifadhi ya San Diego Zoo ilisema katika taarifa.

Lakini inafahamika kuwa kupungua huko kumechangiwa na shughuli kama vile uwindaji, kupungua kwa misitu, ushindani kwa lishe na migogoro ya kila mara yake yao na wafugaji na wakulima.

Pitfold ni miongoni mwa kundi la wataalamu Hifadhi ya Wanyama ya San Diego wanaofanya kazi pamoja na washirika kama vile; Shirika la Wanyama Nchini (KWS), kuchunguza idadi ya chui katika eneo hilo na kusaidi kuwalinda.