Habari Mseto

Chuma ki motoni kwa wanaopachika wanafunzi mimba Murang'a

June 12th, 2019 1 min read

NA SAMMY WAWERU

ZAIDI ya wanaume 20 waliopatikana na hatia ya kupachika wanafunzi mimba katika Kaunti ya Murang’a wamehukumiwa mahakamani.

Waziri wa Afya na Usafi, katika kaunti hiyo Dkt Joseph Mbai pia amesema kuna kesi za wanaume watatu walioshukiwa kupachika wanafunzi wa kike mimba zinaendelea.

Dkt Mbai Jumatano alisisitiza kwamba serikali ya kaunti ya Murang’a haitalegeza kamba vita dhidi ya mimba za mapema.

Alisema itaendelea kukabiliana na wanaume wahuni wanaonyemelea wasichana walio chini ya umri wa miaka 18.

Visa vya wanafunzi Murang’a kutungwa mimba vimeonekana kuongezeka.

Waziri alisema wasichana wengi wanahadaiwa kwa pesa na wanaume aliotaja kuwa ‘sponsa’. “Uchunguzi wetu umebaini wanadanganywa kwa vitu vidogo sana. Ni aibu kuona mzee aliyefikisha miaka 50 akijamiiana na msichana ambaye hajakomaa,” alikashifu Dkt Mbai.

“Ukipachika msichana wa shule mimba kuwa tayari kuelekea jela, tusipofanya hivyo siku za usoni Murang’a itakuwa na kizazi chenye shida chungu nzima,” alionya waziri.

Waziri hata hivyo alieleza kusikitishwa kwake na baadhi ya wazazi waathiriwa wanaokataa kuandikisha taarifa kwa polisi, wakitaka visa vya hivyo visuluhishwe kinyumbani.

Alisema washukiwa huwahadaa kwa fidia, kisha wanapuuza majukumu yao. “Baadhi ya wasichana pia wanakataa kuandikisha taarifa. Kuna wanaojutia hatua ya kutatua mizozo hiyo kinyumbani. Haki ni; mhusika ashtakiwe na kuhukumiwa,” alisema.

Pendekezo la kupunguza umri wa kuruhusu tendo la kujamiiana kutoka miaka 18 hadi 16 linaendelea kualika hisia tofauti, Dkt Mbai akikashifu hatua hiyo. Anasema umri huo usalie ulivyokuwa kwa mujibu wa sheria.

Waziri huyo wa afya na usafi Murang’a alitaja Kiharu, Gatanga na Maragua kama maeneobunge yaliyoathirika zaidi kwa mimba za mapema.

Mwaka uliopita msimu wa mitihani ya kitaifa darasa la nane na kidato cha nne, taifa lilishangazwa na idadi kubwa ya wasichana wajawazito waliofanya mtihani.