Michezo

Chumo achoma wapinzani mbio za Barcelona Half Marathon

February 16th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa mbio za kilomita 15 za Pfixx Solar Montferland nchini Uholanzi, Victor Chumo ndiye mfalme mpya wa mbio za Barcelona Half Marathon mwaka 2020. Ameonyesha wakimbiaji wanaume kivumbi nchini Uhispania, Jumapili.

Mkenya Chumo, 33, alimshinda Mganda Stephen Kissa,25, na Mkenya Moses Koech kwa sekunde mbili pekee katika mbio hizo za kilomita 21 zilizokuwa za kusisimua.

Chumo ni mwanamume wa saba kutoka Kenya kuwa bingwa wa Barcelona Half Marathon baada ya Peter Kosgei (2011), Abel Kirui (2012), Eliud Kipchoge (2013 na 2014), Vincent Kipruto (2016), Leonard Kipkoech (2017) na Eric Kiptanui (2019).

Hakuna mwanamke kutoka Kenya amepata kutwaa taji la Barcelona Half Marathon tangu Florence Kiplagat aponyoke na mataji ya mwaka 2014, 2015, 2016 na 2017. Mwaka 2020, mwanamke wa kwanza kutoka Kenya kufika utepeni alikuwa Dorces Jepchumba Kimeli, 23, katika nafasi ya tatu.

Wakenya wengine ambao wamewahi kunyakua taji la kinadada mjini Barcelona ni Priscah Jeptoo mwaka 2011 na Lineth Chepkurui (2012).

Kiplagat anashikilia rekodi ya wanawake ya Barcelona Half Marathon ya saa 1:05:09 naye Muethiopia Mule Wasihun anajivunia rekodi ya wanaume ya dakika 59:44.

Matokeo (Februari 16, 2020):

Wanaume

Victor Chumo (Kenya) dakika 59:58

Stephen Kissa (Uganda) saa 1:00:00

Moses Koech (Kenya) 1:00:00

Wanawake

Ashete Bekere (Ethiopia) saa 1:06:37

Asnakech Awoke (Ethiopia) 1:07:04

Dorcas Kimeli (Kenya) 1:07:10