Habari Mseto

Chunga usiliwe pesa bure, wazee wamuonya Ruto

January 4th, 2020 2 min read

Na ERIC MATARA

BARAZA la wazee eneo la Rift Valley, limemuonya Naibu Rais William Ruto kuwa macho asipotoshwe na matapeli wa kisiasa wanaojifanya kuwa wanaunga azma yake ya kugombea urais mwaka 2022 ili wapate pesa kutoka kwake.

Wakiongozwa na Mzee Gilbert Kabage, wazee hao walidai kuwa kuna mabroka kwa kisiasa ambao wamekuwa wakitembelea nyumbani kwa Dkt Ruto eneo la Sugoi na Karen jijini Nairobi kupata pesa tu na kumfilisisha.

“Naibu Rais anapaswa kufahamu kuwa kuna mabroka wa kisiasa na matapeli wanaojihusisha naye kupata pesa tu. Dkt Ruto amejaliwa uwezo wa kifedha na kwa hivyo matapeli wa kisiasa wanaelekea kwake kupata pesa. Wengi wa viongozi hawa hawamuungi mkono katika mioyo yao, wanachotaka ni kujitajirisha binafsi na kulemaza azima yake ya kisiasa,” alisema Bw Kabage.

Wazee hao walisema matapeli hao wamekuwa wakimpotosha Dkt Ruto na watahujumu azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“Naibu Rais anapaswa kujihadhari na watu hao ambao watamhepa baada ya kupata pesa ya kutimiza maslahi yao ya kisiasa. Wengi wao ni walaghai na wanaojali matumbo yao na hawana thamani yoyote kwa azima yake ya kuwa rais wa nchi hii,” aliongeza Bw Kabage.

Kauli ya viongozi hao inajiri chini ya mwezi mmoja baada ya mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri, kuongoza ujumbe wa viongozi kutoka jamii ya Wakikuyu kutoka kaunti za Nakuru, Nyandarua na Laikipia nyumbani kwa Dkt Ruto, Sugoi, kaunti ya Uasin Gishu. Kwenye mkutano huo, viongozi walijadili masuala mbali mbali ikiwa ni pamoja na uchaguzi mkuu wa 2022.

Kabla ya kukutana na Dkt Ruto, viongozi hao walikutana na wenzao kutoka jamii ya Wakalenjin katika hoteli moja mjini Eldoret.

Waliohudhuria mkutano huo waliahidi kumuunga mkono Dkt Ruto kugombea urais kwenye uchaguzi wa 2022.

Hata hivyo, Ijumaa, Bw Kabage na wazee wenzake walimtaja Bw Ngunjiri kama mwanasiasa anayejali maslahi yake pekee na wakamuonya dhidi ya kudai kwamba anawakilisha jamii ya Wakikuyu eneo la Rift Valley.

“Sisi kama wazee wa Wakikuyu katika Rift Valley, tunaunga mkono azima ya Dkt Ruto lakini tuna wasemaji wetu na Bw Ngunjiri na walioandamana naye hawazungumzi kwa niaba yetu,” alisema.

Walisema Bw Ngunjiri anampotosha Dkt Ruto kwa kujifanya msemaji wa Wakikuyu wanaoishi Rift Valley.

Ruto atajwa mwanasiasa shupavu

Walisema kwamba wako na hakika Dkt Ruto atavuka vizingiti vyote na kumrithi Rais Kenyatta.

Mzee mwingine Bw Peter Koech alisema Dkt Ruto ni mwanasiasa shupavu na hatategemea kutawazwa na vigogo wengine wa siasa ili kushinda urais.

“Ni Dkt Ruto aliyemsaidia Rais Uhuru Kenyatta kwenye chaguzi za 2013 na 2017. Ni yeye aliyemsaidia aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2007 na kwa hivyo hatahitaji kuidhinishwa na vigogo wa kisiasa kwa sababu tayari anaungwa na Wakenya wengi mashinani,” alisema.