Habari Mseto

Chuo Kikuu cha Mama Ngina kujengwa Gatundu Kusini

April 16th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa eneo la Gatundu Kusini watanufaika kutokana na uzinduzi wa ujenzi wa Chuo Kikuu kitakachotoa elimu ya juu kuwafaa si tu wakazi wa eneo hilo bali kwa wote wanaostahili.

Chuo hicho cha Mama Ngina University, kitaendelea kujengwa katika kijiji cha Mutomo, anakotoka Rais wa nchi, Uhuru Kenyatta.

Kitaanza kikiwa bewa la Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Chuo hicho kitagharimu takribani Sh2 bilioni na kinatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka wa 2022.

Chuo hicho kiliangaziwa kujengwa na aliyekuwa wakati mmoja Mbunge wa Gatundu Kusini mwaka wa 2013, marehemu Joseph Ngugi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo mwishoni mwa wiki jana, Chansela wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, Dkt Benson Wairegi, alisema kuwa wakati Chuo hicho kitakapokamilika, kitawasajili wanafunzi wapatao 10,000 kwa mara ya kwanza.

Alisema chuo hicho cha Mama Ngina, ambacho kitakuwa na ushirikiano na KU, kitaweza kuvutia wanafunzi wengi kutoka kila eneo la nchi.

“Tunatarajia kusajili wanafunzi wengi kutoka pembe zote za nchi na hatutakuwa na ubaguzi wowote wakati wa shughuli kama hiyo,” alisema Dkt ¬†Wairegi.

Mbunge wa Gatundu Kusini ambaye alihudhuria uzinduzi huo, Bw Moses Kuria, alisema chuo hicho kitaleta maendeleo hasa katika eneo hilo huku wakazi wengi wakipata ajira.

“Ninafurahi kusema ya kwamba sura ya Gatundu Kusini itageuka pakubwa huku ikipata wageni wengi kutoka miji mingine,” alisema Bw Kuria.

Alisema changamoto kubwa katika eneo la Gatundu ni ukosefu wa nyumba za kuishi, na kwa hivyo akapendekeza serikali kuingilia kati na kufuatilia mojawapo ya ajenda nne muhimu za serikali ambayo ni ujenzi wa majumba.

Alisema wafanyakazi wengi ambao hufanya kazi Gatundu Kusini huishi maeneo ya Thika, Ruiru, Juja, na Kenyatta Road kwa sababu ya ukosefu wa makazi ya kuvutia.

“Ninawahimiza wawekezaji kutoka maeneo mengine waje Gatundu ili waanzishe biashara hasa kwa kujenga nyumba za kukodisha,” alisema Bw Kuria.

Uhai kibiashara

Naibu Chansela wa Chuo cha Kenyatta, Prof Paul Wainaina alitoa mwito kwa Kaunti ya Kiambu kufanya juhudi kuleta Maendeleo kwa wingi katika kijiji cha Mutomo ili kulipa eneo hilo uhai wa kibiashara.

“Chuo chetu kitashirikiana na Kaunti ya Kiambu na washika dau wengine kuona ya kwamba tunajadiliana maswala ya Maendeleo hasa ya kibiashara, na usafiri,” alisema Prof Wainaina.

Alisema maswala muhimu yanayostahili kujadiliwa kwa kina ni usambazaji wa maji, umeme, na barabara nzuri.

“Nina uhakika iwapo mambo hayo yote yatazingatiwa kikamilifu bila shaka Gatundu utakuwa mji wa kutembelewa na wageni wengi kutoka maeneo mengi.”

Alisema wakazi wa Gatundu wana imani kubwa ya kwamba wakati Chuo hicho kitakapokamilika miaka mitatu ijayo, vijana wengi watanufaika na ajira kwa wingi, ikizingatiwa ni eneo ambako Rais Kenyatta anatoka.

Wafanyakazi watazama tingatinga linalochota mchanga kwenye eneo la uzinduzi wa Chuo Kikuu cha Mama Ngina, Gatundu Kusini ambacho kitaanza kama bewa la Chuo Kikuu Cha Kenyatta (KU). Picha/ Lawrence Ongaro