Habari Mseto

Chuo Kikuu cha Moi kukwama wafanyakazi, wahadhiri wakitishia kugoma


SHUGHULI zote katika Chuo Kikuu cha Moi, huenda zikalemazwa baada ya wafanyakazi kutishia kugoma kwa kucheleweshewa mishahara na marupurupu mengine.

Chama cha Wahadhiri wa Chuo Kikuu hicho (UASU) kimeungana na kile cha Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (KUSU) na cha wafanyakazi wa Nyumbani, Hoteli, Taasisi za Elimu na Hospitali (Kudheiha) kutoa ilani ya kugoma iwapo hawatalipwa mishahara yao.

“Uasu inatoa ilani ya siku saba ya mgomo kwa Baraza la Chuo Kikuu cha Moi kwa kutolipa wahadhiri mishahara ya Julai kwa viwango vilivyojadiliwa katika Makubaliano ya Pamoja ya mwaka wa 2017-2021,” alisema Dkt

Constantine Wasonga Opiyo, Katibu Mkuu wa kitaifa wa Uasu katika ilani aliyotoa Agosti 19, 2024.

Wanachama wa Kusu na Kudheiha walio wafanyakazi wa Chuo Kikuu hicho pia wametishia kugoma wakilalamikia kucheleweshewa mishahara, kutowasilishwa kwa pesa walizokatwa kulipia mikopo, pensheni na ada zingine.

Wanataka usimamizi na baraza la chuo hicho kubadilishwa wakidai umekisimamia vibaya.