Habari

Chuo Kikuu chalisha familia katika mtaa wa mabanda

June 25th, 2020 1 min read

Na DIANA MUTHEU

WATU 100 kutoka vitongoji duni katika wadi ya Tudor, Mombasa wamefaidika na chakula cha msaada kilichotolewa na Chuo Kikuu cha Ufundi cha Mombasa (TUM).

Wakazi hao ambao walifika katika chuo hicho kupokea chakula Jumatano asubuhi walilalamika kuwa ukosefu wa kazi ambao umechangiwa na janga la corona umewalazimu kulala njaa kwa siku kadhaa.

Akizungumza na Taifa Leo, mama wa watoto watano Bi Chonzi Amaye anayeishi katika mtaa wa mabanda wa Burukenge, katika wadi hiyo ya Tudor, aliwashukuru wasimamizi wa chuo hicho kwa msaada huo wa chakula.

“Kabla ya kukumbwa na janga hili, nilikuwa nafanya vibarua kama vile kufulia watu nguo, lakini kwa sasa siwezi pata kazi hizo kwa kuwa wateja wangu hawawezi kuniruhusu niingie nyumbani kwao, kwa hofu labda nina virusi vya corona,” akasema Bi Amaye.

Naibu Chansela wa taasisi hiyo, Prof Laila Abubakar, alisema kuwa wanapanga kusambaza chakula hicho kwa familia 1,000

“Watu wengi wamepoteza ajira tangu ulimwengu mzima ukumbwe na janga la corona. Tumeona ni vizuri tuwakumbuke majirani zetu wanapopitia wakati huu mgumu,” akasema Prof Abubakar.

Prof Abubakar alisema wakazi kutoka vitongoji duni kama vile sehemu za Beurukenge na Moroto watapewa kipaumbele katika mpango huo wa kutoa chakula hicho.

Pia alisema wakazi wengine wanaoishi karibu na matawi mengine ya chuo hicho katika kaunti za Kwale na Lamu watafaidika.

“Baadhi ya watu wanalala njaa na ni vizuri tusaidiane. Chakula hiki kitawafaa kwa wiki mbili au mwezi mmoja kulingana na ukubwa wa familia,” akasema.

Baadhi ya bidhaa walizopata wakazi ni sabuni, majani, unga wa ngano na wa sima, pojo miongoni mwa zingine.

Naibu Chansela huyo aliwatahadharisha wakazi katika vitongoji duni kutupilia mbali uvumi na dhana potovu kuwa hakuna corona, bali waendelee kujikinga.

“Janga la corona lipo na sote lazima tutahadhari,” akasema Prof Abubakar.