Habari za Kitaifa

CIPK yaomba serikali kutopuuzilia mbali mkataba na madaktari

April 8th, 2024 2 min read

NA TITUS OMINDE

BARAZA la Maimam na Wahubiri Nchini (CIPK) limesihi serikali kutopuuza Mkataba mzima wa Makubaliano ya Pamoja (CBA) kati ya Wizara ya Afya na madaktari, na badala yake itekeleze angalau asilimia 80 ya makubaliano hayo. 

Mwenyekiti wa CIPK Sheikh Abubakar Bini alisema ikiwa serikali itadumisha msimamo wake mkali kama alivyosisitiza Rais William Ruto, huduma za afya zitakuwa hatarini.

Sheikh Bini alisema ikiwa CBA nzima haitatekelezwa, madaktari na wahudumu wengine wa afya watadhoofika hivyo Wakenya kuhangaika kupata huduma.

“Mkataba kati ya wizara ya afya na madaktari ni haki kisheria na ikiwa serikali itapuuza CBA nzima, itakuwa kinyume cha sheria na Wakenya maskini wanaolipa ushuru ndio watapata taabu kwa vile madaktari na matabibu wengine watavunjika moyo na hivyo kutoa huduma duni kwa Wakenya,” alisema Sheikh Bini.

Akizungumza katika Madras ya Eldoret wakati wa usambazaji wa chakula cha msaada kwa Waislamu waliofunga kabla ya IDD-UL -FITRI, Sheikh Bini alisema ikiwa madaktari watapunjwa hawatatoa huduma bora kwa Wakenya.

Kiongozi huyo wa kidini aliwataka washikadau wote wakiongozwa na Rais Ruto kukumbatia mazungumzo ili kusuluhisha mvutano uliopo.

Kiongozi huyo alimtaka Dkt Ruto kuongoza mdahalo huo akidai ni wazi kuwa Waziri wa Afya Susan Nakhumicha anaonekana kushindwa kuzungumza na madaktari wanaogoma.

Hata hivyo, alisisitiza haja ya pande zinazohusika kulegeza misimamo yao akipendekeza kutekeleza angalau asilimia 80 ya mkataba huo.

“Pamoja na msimamo uliochukuliwa na Rais akiambia madaktari kwamba wanapaswa kuishi kulingana na uwezo wao kifedha, serikali inapaswa kuwa adilifu na aminifu kwa madaktari kwa kutekeleza angalau asilimia 80 ya mkataba badala ya kupuuza makubaliano yote,” alisema Sheikh Bini.

Sheikh Bini alielezea matumaini kuwa ikiwa Rais Ruto atachukua hatua ya kijasiri ya kuwa na mazungumzo na madaktari, mgomo unaoendelea utakuwa historia.

Alisema kuwa Kenya ina raslimali za kutosha kulipa madaktari vyema lakini changamoto ni ufisadi na kutopewa kipaumbele matakwa muhimu.

“Wanjiku hulipa ushuru ili kupokea huduma bora lakini ufisadi umefanya hali kuwa ngumu ambapo ushuru wa Wakenya hautumiki vyema. Kenya ina rasilimali za kutosha kulipa madaktari wote vizuri, lakini changamoto kubwa ni ufisadi na kuipa kipaumbele huduma muhimu kama vile afya,” alisema Sheikh Bini.

Tayari wataalamu wa afya wamesema kuwa kukosekana kwa mwafaka kwa masaibu yao kunahatarisha utekelezwaji wa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC) iliyoanza 2018 kama majaribio katika kaunti nne za Nyeri, Isiolo, Machakos na Kisumu.

“Tunaomba kwa dharura mamlaka husika kuheshimu ahadi yao, kwa kutanguliza ustawi wa madaktari wetu, na kuchukua hatua za haraka kutekeleza mkataba wetu, kuhakikisha kwamba mifumo yetu ya afya inaweza kuwahudumia wale wanaohitaji,” Katibu mkuu wa KMPDU Dkt Davji Atellah alisema wakati wa mkutano wake na madaktari wanaogoma mjini Eldoret wiki jana.

Msimamo sawa umetolewa na kasisi Joseph Otondo Mwangalizi wa makanisa Pentecostal Assemblies of God (PAG).

“Inatisha kwamba wale wanaofanya kazi kwa bidii kulinda afya zetu kupuuzwa, serikali ijadiliane na madaktari kwa njia ya heshima kwa ajili ya kulindwa Wakenya,” alisema Kasisi Otondo.

Hata hivyo Rais Ruto amesisitiza kuwa serikali haina pesa za kuongeza mishahara ya madaktari.

Akizungumza Jumapili baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa la Eldoret AIC Fellowship, rais Ruto alisema nchi inatumia Sh trilioni 1.1 kila mwaka kati ya trilioni 2.2 zinazokusanywa kwa malipo ya mishahara na mishahara.

Aliwambia madaktari wanaogoma kuhusu madai ya nyongeza ya mishahara na marupurupu ya wanafunzi, akisema nchi inakabiliana na bili kubwa ya mishahara hivyo basi serikali inafanya kila juhudi kukabiliana na changamoto husika.