Michezo

Ciro Immobile anusia rekodi ya ufungaji barani Ulaya

July 30th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MATUMAINI ya Cristiano Ronaldo kuibuka mfungaji bora katika soka ya bara Ulaya msimu huu yalididimia zaidi mnamo Julai 29, 2020, baada ya kushindwa kutikisa nyavu za wapinzani katika mchuano ulioshuhudia waajiri wake Juventus wakichapwa 2-0 na Cagliari.

Nyota huyo matata mzawa wa Ureno anajivunia mabao 31 kutokana na kampeni za Ligi Kuu ya Italia (Serie A) hadi kufikia sasa msimu huu.

Licha ya Juventus kuonekana kutamalaki mechi na kuwazidi maarifa wapinzani wao katika takriba kila idara, ni Cagliari ndio waliotumia vyema uwanja wao wa nyumbani na kuvuna ushindi muhimu.

Mabao ya kikosi hicho yalifumwa wavuni na Luca Gagliano na Giovanni Simeone katika dakika ya nane na 45 mtawalia.

Ronaldo kwa sasa anahitaji mabao manne zaidi ili kumfikia Ciro Immobile wa Lazio katika vita vya kuwania taji la mfungaji bora miongoni mwa wanasoka wote wa ligi za bara Ulaya msimu huu.

Immobile alifunga bao lake la 35 msimu huu mnamo Jumatano ya Julai 29 katika mechi iliyowashuhudia Lazio wakiwapepeta Brescia 2-0.

Ikisalia mechi moja pekee kabla ya kampeni za Serie A kutamatika rasmi msimu huu, Immobile ndiye anapigiwa upatu kuibuka mfungaji bora wa bara Ulaya.

Bao lake la hivi karibuni lilimwezesha kumpiku Robert Lewandowski wa Bayern Munich aliyefunga rasmi kampeni za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa magoli 34.

Immobile kwa sasa anasalia na bao moja pekee kufikia rekodi ya Gonzalo Higuain aliyewahi kufunga idadi kubwa zaidi ya mabao katika msimu mmoja wa Serie A.

Higuain alipachika wavuni mabao 36 akivalia jezi za Napoli mnamo 2015-16.

MATOKEO YA SERIE A (Julai 29, 2020):

Cagliari 2-0 Juventus

Lazio 2-0 Brescia

Sampdoria 1-4 AC Milan

Sassuolo 5-0 Genoa

Udinese 1-2 Lecce

Verona 3-0 Spal

Fiorentina 4-0 Bologna

Torino 2-3 Roma