Michezo

Ciro Immobile mfungaji bora wa Serie A

August 4th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI Ciro Immobile, 30, alitawazwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na akaibuka pia mfumaji bora miongoni mwa wanasoka wote wa Ligi Kuu ya za bara Ulaya msimu huu wa 2019-20.

Nyota huyu mzawa wa Italia alicheka na nyavu katika mechi iliyoshuhudia waajiri wake Lazio waliomaliza kampeni za msimu huu katika nafasi ya nne jedwalini, wakipepetwa 3-1 na Napoli mnamo Agosti 1, 2020.

Bao la Immobile ambaye pia amewahi kuchezea Borussia Dortmund na Sevilla, lilimwezesha kuifikia rekodi ya fowadi mzawa wa Argentina, Gonzalo Higuain aliyepachika wavuni jumla ya magoli 36 mnamo 2015-16 akivalia jezi za Napoli. Higuain, 32, kwa sasa huchezea Juventus ya Italia.

Fabian Ruiz aliwaweka Napoli kifua mbele kunako dakika ya tisa kabla ya Immobile kusawazisha mambo dakika 13 baadaye. Mabao mengine kutoka kwa Lorenzo Insigne na Matteo Politano yaliwezesha Napoli ya kocha Gennaro Gattuso kutia kapuni alama zote tatu zilizowadumisha katika nafasi ya saba kwa alama 62, nane nyuma ya AS Roma waliofunga mduara wa tano-bora.

Cristiano Ronaldo aliyepumzishwa na Juventus katika mchuano wao wa mwisho dhidi ya Roma, aliambulia nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji bora wa Serie A kwa mabao 31, manane zaidi kuliko Romelu Lukaku wa Inter Milan.

Immobile alikamilisha kampeni za msimu huu katika soka ya bara Ulaya kwa mabao mawili zaidi kuliko Robert Lewandowski aliyewafungia Bayern Munich jumla ya magoli 34. Ronaldo aliambulia nafasi ya tatu.

Ilikuwa mara ya tatu kwa Immobile kutwaa taji la mfungaji bora wa Serie A baada ya kulitia kapuni mnamo 2013-14 alipopachika wavuni jumla ya magoli 22 kisha kulinyanyua kwa pamoja na Mauro Icardi mnamo 2017-18 kila mmoja wao alipocheka na nyavu mara 29.

Hii ni mara ya kwanza tangu 2006-07 kwa taji la mfungaji bora katika soka ya bara Ulaya kutomwendea mchezaji asiye wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga). Taji hilo lilitwaliwa na Francesco Totti wa Roma mnamo 2006-07.

Lionel Messi wa Barcelona aliyeibuka mshindi wa taji hilo katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita alifaulu kutikisa nyavu za wapinzani mara 25 pekee muhula huu wa 2019-20.