Michezo

CITY NDANI: Mambo mazuri kwa Manchester City

November 28th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

BAADA ya Manchester City kutinga hatua ya 16 Bora ya michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya, kocha wa timu hiyo ameahidi kuelekeza macho yake kwa kinyang’anyiro cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

City ambao sasa wanaongoza kundi lao la C wafuzu kwa hatua hiyo licha ya kutoka sare 1-1 na Shakhtar Donestk ya Ukraine kwenye mechi iliyochezewa Itihad, Jumanne usiku.

Ilkay Gundogan alifungia wenyeji bao hilo, huku Donetsk wakipata lao kupitia kwa Manor Solomon.

“Lengo letu lilikuwa kufuzu kwa hatua ya maondoano na sasa tumefanya hivyo,” alisema Guardiola, ambaye aliisaidia Barcelona kutwaa ubingwa wa bara mara mbili.

“Michuano hii itakuwa tofauti kabisa na ngumu kuanzia mwezi Februari, lakini tutasubiri kuona tutakavyofika pale. Ni michuano ambayo inahitaji umakinifu mkubwa zaidi.”

“Michuano ya makundi inachanganya lakini sasa shindano moja limemalizika- tutacheza mechi ya mwisho tukiwa kileleni mwa msimamo- na sasa tunaweza kuelekeza mawazo yetu kwa EPL hadi wakati ratiba ya UEFA itakaporejelewa.”

City, ambao wametwaa ubingwa wa EPL katika misimu miwili iliyopita, kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini, kwa mwanya wa pointi tisa nyuma ya Liverpool.

Kutokana na kuwepo kwao katika michuano ya Carabao Cup, kikosi cha Guardiola kikicheza mechi tisa kuanzia Novemba 30 hadi December, ingawa sasa watapata fursa ya kupumzisha wachezaji watakapocheza mechi ya mwisho ya UEFA dhidi ya Dinamo Zagreb ya Croatia mnamo Disemba 11.

Donetsk ambao walikuwa wamefungwa mabao 12-0 na City katika mechi tatu za awali, wakati huu walicheza kwa kiwango cha juu.

City ambao walicheza bila mshambuliaji wao tegemeo Sergio Aguero anayeuguza jeraha la paja, hawakuwa wakali katika safu ya ushambuliaji kama ilivyotarajiwa, licha ya pasi kadhaa kutoka kwa kiungo Kevin de Bruyne.

Hata Jesus aliyepewa nafasi ya Aguero hakuonyesha makali yoyote licha ya kupokea pasi nyingi pamoja na David Silva.

Kwa mashabiki wa City, mchezo wa kikosi chao hakikuwaridhisha hasa wakati huu ligi kuu nchini Uingereza imechacha.

Inakumbukwa kwamba City waliandikisha ushindi mkubwa wa 6-0 dhidi ya Shakhtar miezi 12 iliyopita, lakini walishindwa kuvuma mbele ya mashabiki wao Jumanne.

Shakhtar Donetsk wameshinda mechi moja kati ya tano kwenye kundi hili lakini wanakamata nafasi ya pili na watafuzu iwapo wataishinda Atalanta.

Baada ya matokeo ya Jumanne, Manchester City wanajivunia rekodi ya kutoshindwa katika mechi 10 za makundi katika michuano ya UEFA (wameshinda saba na kutoka sare mara tatu), tangu Septemba 2018 (kikiwemo kichapo cha 2-1 kutoka kwa Shakhtar Donetsk mnamo Decemba 2017).

Shakhtar Donetsk wametoka sare mara tatu mfululizo katika michuano hii kwa mara ya kwanza, kadhalika wameenda mechi nne mfululizo ugenini bila kushindwa baada ya kushinda mara mbili na kutoka sare mara mbili.