Michezo

CITY PEMA: City yatarajiwa kuweka hai matumaini FA ikisakata na Brighton

April 6th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

MANCHESTER City inapigiwa upatu kuwa mwiba kwa wapinzani wao Brighton katika nusu-fainali ya Kombe la FA uwanjani Wembley inapofukuzia kuweka hai matumaini ya kunyakua mataji manne msimu huu.

Karibu mechi 13 zinatengenisha vijana wa Pep Guardiola na ufanisi wa mataji ya FA, Ligi Kuu na Klabu Bingwa Ulaya kuongeza kwa ubingwa wa kipute cha League Cup ambao walitwaa mwezi Februari.

Hata hivyo, huku mechi saba zikisubiri City mwezi Aprili, Guardiola anakabiliwa na tatizo katika nafasi moja.

Oleksandr Zinchenko alipata jeraha la mguu katika ushindi wa City wa mabao 2-0 dhidi ya Cardiff kwenye Ligi Kuu mnamo Jumatano.

Beki huyu wa Ukraine amefanya vyema majukumu ya kuziba pembeni kushoto, licha ya kuwa yeye alikuwa kiungo kabla ya Guardiola kuwasili, huku mshindi wa Kombe la Dunia Benjamin Mendy akiwa mkekani kutokana na majeraha ya magoti katika misimu miwili.

Uvumilivu wa Guardiola kwa Mendy umepungua sana na alijaribiwa tena juma hili pale beki huyu alipopigwa picha katika kilabu moja cha usiku saa tisa na nusu asubuhi Jumamosi iliyopita, saa chache kabla ya mabingwa wa Uingereza kusafiri hadi Fulham.

Mendy hakuwa katika kikosi cha kusakata mechi siku hiyo, lakini alitarajiwa kushiriki mazoezi siku iliyofuata ili kuendelea na matibabu yake.

“Wana akili za kutosha kujua wao ni watu wazima, mimi si baba yao,” alisema Guardiola alipoulizwa ikiwa alikerwa na Mendy kupatikana kilabuni usiku wa manane.

Mendy amecheza dakika 27 pekee katika mechi ya League Cup dhidi ya timu kutoka daraja ya tatu Burton Albion tangu mwezi Novemba na Guardiola awali alisema kuhusu kuongeza nguvu katika safu ya nyuma pembeni kushoto kwa msimu ujao, ishara kwamba nafasi ya Mfaransa huyo si salama.

Huku Fabian Delph pia akiwa nje akiuguza jeraha, Mendy huenda akaorodheshwa kusakata kucheza kutokana na ratiba ya mechi nyingi ambayo City inayo, Guardiola akikiri kwamba “hatuna vizibo vingi.”

Baada ya kukabiliana na timu ya Brighton inayotafuta kufika fainali ya FA kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 36, City italimana na Tottenham mara tatu katika kipindi cha siku 10 kabla ya kusafiri hadi Crystal Palace, Manchester United na Burnley baadaye Aprili.

Brighton inapigania kusalia Ligi Kuu, lakini kocha wake Chris Hughton anasisitiza kwamba inaweza kushangaza City, hata kama itakuwa “ujinga kupambana” na vijana wa Guardiola.

Sterling arejea

Raheem Sterling, ambaye amefungia City mabao manane katika mechi sita zilizopita, anarejea katika mechi hii baada ya kupumzishwa katikati mwa wiki.

Atakuwa muhimu katika kampeni ya City kumaliza ukame wa mataji ya FA, ambayo ilishinda mara ya mwisho mwaka 2011.
Brighton, ambayo imepoteza mechi nne mfululizo dhidi ya City, inatarajiwa kumtegemea Glenn Murray kutupa miamba hawa nje.