Michezo

City Queens wapepetwa na Kibagare Girls

April 2nd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya City Queens ilidhalilishwa kwa mabao 4-0 na Kibagare Girls kwenye mechi ya Nairobi West Regional League (NWRL) iliyosakatiwa uwanja wa KNH, Nairobi.

Nayo Patriots Queens ililazimika kuachia alama zote licha ya kuongoza kwa mabao 2-1 dhidi ya Uweza Women baada ya wapinzani hao kuondoka Uwanjani wakidai wenzao hawakuonyesha stakabadhi zote muhimu.

Kibagare Girls chini ya nahodha, Dorothy Gimase ilishusha mchezo safi na kulipiza kisasi baada ya kuzimwa kwa bao 1-0 na Uweza Women wiki mbili zilizopita.

Vigoli hao walitwaa ufanisi huo kupitia juhudi zake Jane Otieno aliyepiga mbili safi, huku Irene Khatiala na Sarah Machuka wakiitingia bao moja kila mmoja.

”Nashukuru wasichana wangu kwa kazi njema pia kuvuna alama zote tena kwa ushindi mnono hali inayoashiria wamepania kufanya vyena msimu huu,” kocha wa Kibagare Girls, Joseph Itotia alisema na kuwahimiza kutolaza damu.

Nayo Lifting the Bar awali ikifahamika kama Beijing Raiders iliikomoa UoN Queens kwa mabao 2-0.

Kwenye jedwali, Uweza Women imetwaa uongozi wa mapema kwa alama tisa baada ya kucheza mechi tatu. Nayo Kibagare ya pili kwa alama tatu sawa na Lifting the Bar, Amani Queens na Carolina for Kibera tofauti ikiwa idadi ya mabao.