Michezo

CITY SIMBA MAJERUHI: Manchester City kupambana na Watford

September 21st, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

SAWA na simba majeruhi, baada ya Manchester City kuteleza mikononi mwa limbukeni Norwich katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza juma lililopita, mabingwa hao watetezi watakuwa makini kumalizia udhia wao kwa Watford uwanjani Etihad, leo Jumamosi.

City, ambao waliduwazwa kwa mabao 3-2 na Norwich na kuachwa kwa alama tano na mabingwa wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Liverpool, wataingia uwanjani na rekodi ya kushinda Watford katika mechi 11 zilizopita.

Vijana wa kocha Pep Guardiola, ambao wanashikilia nafasi ya pili kwenye jedwali, watakutana na Watford, ambayo bado inatafuta ushindi wa kwanza msimu huu baada ya kuanza na vichapo vitatu na kupiga sare katika mechi mbili zilizopita.

Hata hivyo, City itajipata pabaya kama haikujifunza kutokana na Arsenal kuhangaishwa na Watford katika kipindi cha pili hadi dakika ya mwisho katika sare ya 2-2 dhidi ya vijana hao wa Unai Emery.

Mshambuliaji Raheem Sterling huwa mwiba kwa Watford. Ameifunga mabao sita katika mechi tano zilizopita.

Mwingereza huyo anatarajiwa kuwa mmoja wa wachezaji City itategemea kutafuta kuziba mwanya kati yake ya Liverpool, ambayo itapimwa makali yake na Chelsea hapo kesho.

City inakabiliwa na uhaba wa mabeki baada ya John Stones kuingia katika orodha ya majeruhi juma hili. Tegemeo Aymeric Laporte yuko nje miezi sita akiuguza jeraha.

Matatizo katika safu ya ulinzi ya City yanaweza kuwa baraka kwa Watford ikivumbua jinsi ya kukabiliana na washambuliaji matata Sterling, Sergio Aguero na Gabriel Jesus na wakati huo huo ikiimarisha mashambuliaji yake.

Takwimu zinaonesha Watford inavuja na pia inatatizika kupata mabao. Imefunga mabao manne pekee na kufungwa 10 katika mechi tano ligini. Aguero anaongoza katika ufungaji wa mabao msimu huu baada ya kutikisa nyavu mara saba.

Kiungo Fernandinho ameimarisha kidogo safu ya ulinzi ya City baada ya Guardiola kuamua kumtumia katika nafasi hiyo. Mchango wa Brazil huyo katika idara hiyo ulidhihirika ikilipua Shakhtar Donetsk 3-0 nchini Ukraine kwenye Klabu Bingwa katikati mwa juma.

Watford ya kocha Quique Sanchez Flores imeonyesha inaweza kuwa hatari. Hata hivyo, tegemeo wake Troy Deeney, Will Hughes, Abdoulaye Doucoure, Tom Cleverley, Christian Kabasele na Daryl Janmaat watalazimika kufanya kazi maradufu kuvuna alama uwanjani Etihad, ambamo timu yao ilikung’utwa 6-0 ilipoutembelea mara ya mwisho mwezi Mei katika Kombe la FA.

Jumla ya mechi tano zitasakatwa leo Jumamosi.

Leicester itakaribisha Tottenham uwanjani King Power ikilenga kufuta kichapo cha bao 1-0 ilichopata kutoka kwa Manchester United wiki moja iliyopita.

Ni mechi inayotarajiwa kuwa ngumu. Tottenham, ambayo Mkenya Victor Wanyama anasubiri kuanza mechi yake ya kwanza baada ya uhamisho wake kukwama, ilipepeta Crystal Palace 4-0.

Everton itakuwa mwenyeji wa Sheffield United katika mechi ambayo timu zote mbili zinauguza vichapo kutoka kwa Bournemouth na Southampton, mtawalia.

Mechi kati ya Newcastle na Brighton uwanjani St James Park itakuwa vita vya timu zinazofanya vibaya.

Brighton haina ushindi katika mechi nne mfululizo nayo Newcastle haijashinda mechi mbili zilizopita.

Burnley itaalika Norwich ikitumai kufuta kipigo cha mabao 4-1 ilichopokea pale zilipokutana mara ya mwisho mwaka 2012.

Burnley ilifungua msimu kwa kuchabanga Southampton 3-0, lakini haijapata ushindi tena.