City Stars, Homeboys na Bandari zawika ligi ikianza kushika kasi

City Stars, Homeboys na Bandari zawika ligi ikianza kushika kasi

Na CECIL ODONGO

Nairobi City Stars, Kakamega Homeboyz na Bandari zimechukua uongozi wa mapema wa msimu, Ligi Kuu nchini baada ya kutwaa nafasi tatu za kwanza mtawalia kwa alama tisa.

Kati ya timu hizo tatu, Homeboyz bado haijafungwa bao lolote na wikendi iliendeleza matokeo bora kwa kuvunja rekodi ya kutoshindwa kwa Posta Rangers, ilipoizaba 2-0 ugani Bukhungu Kaunti ya Kakamega.

Chini ya Kocha mpya Bernard Mwalala ambaye alirithi mikoba ya ukufunzi kutoka kwa Nicholas Muyoti, Homeboyz ilisajili matokeo ya 1-0 dhidi ya Police FC nyumbani mechi ya kwanza ya msimu kabla ya kuipiga Wazito pia 1-0 ugenini.

“Bado ni mapema sana kusema kuwa sisi ndio tutashinda taji la ligi kuu. Wachezaji wangu wamekuwa wakijituma sana uwanjani ila bado kuna timu ngumu zaidi ambazo tutakutana nazo ligi ikiendelea,” akasema Mwalala baada ya ushindi huo.

Nairobi City Stars inayoongoza ligi hiyo ilipata ushindi wa 2-0 dhidi ya Bidco huku Bandari ikizidisha masaibu ya AFC Leopards baada ya kuipiga 2-1 ugani Mbaraki.Huku dirisha dogo la uhamisho wa wachezaji likikaribia kufungwa mnamo Novemba 1, mkufunzi wa Leopards raia wa Ubelgiji Patrick Aussems amesema kuwa Ingwe itakuwa pabaya isiponunua mshambuliaji hodari.

Ingwe iliishangaza mabingwa watetezi Tusker 1-0 katika mechi ya ufunguzi mnamo Septemba 26 kabla ya kuenda sare tasa dhidi ya KCB majuma mawili yaliyopita.KCB na FC Talanta nazo zilipata ushindi wao wa kwanza msimu huu baada ya kuilemea Sofapaka 2-1 na Vihiga Bullets 1-0 mtawalia katika nyuga za Thika na MISC Kasarani mtawalia.

Wazito, Bidco United, Nzoia Sugar, Vihiga Bullets na Tusker ndizo timu ambazo bado hazijasajili ushindi wowote tangu msimu uanze ila vijana wa kocha Robert Matano wamecheza mechi moja pekee kwa kuwa walikuwa wakiwajibikia mechi za Caf.

You can share this post!

MARY WANGARI: Mauaji ya Tirop ni uhalisia mchungu wa janga...

DKT FLO: Mbinu asili za kuzuia kisukari ni salama?

T L