Michezo

City Stars, Nairobi Stima zazidi kutamba soka ya BNSL

December 9th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Nairobi City Stars iliendelea kufyeka wapinzani wao kwenye mechi ya kufukuzia taji la Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL) uwanjani Camp Toyoyo Jericho, Nairobi.

Nao vijana wa Nairobi Stima walisalia katika nafasi ya pili licha ya kutoka sare tasa na Bidco United ya tatu kwenye jedwali.

City Stars ya kocha, Sanjin Alagin inaendelea kugawa dozi dhidi ya wapinzani wao msimu huu ikitafuta tiketi ya kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki soka la Ligi Kuu ya KPL.

Kati ya wanasoka mahiri wa kikosi hicho, Davis Amuyunzu na Anthony Kimani walichochea wenzao dimbani na kubeba City Stars kutia kapuni alama zote muhimu.

”Hatuna la ziada bali tumepania kuendeleza mtindo wa kuwachoma wapinzani wetu kwenye mechi zetu sijazo ili kujiweka pazuri kutoa mfukoni tiketi ya kusonga mbele,” meneja wa City Stars, Neville Pudo alisema.

Nayo Ushuru FC iliteleza na kushindwa kuzima jitihada za wenyeji wao ilipotoka sare bao 1-1 na Modern Coast Rangers huku Migori Youth ikilala kwa mabao 3-2 mbele ya Shabana FC.

Shabana chini ya naibu kocha, Vincent Nyaberi ilitwaa ufanisi huo muhimu baada ya kupoteza mechi kadhaa kwenye kampeni hizo. Kocha huyo alisema huduma zao Fredrick Nyakundi na John Omondi zilisaidia pakubwa kikosi kuvuna ushindi wa pointi tatu muhimu.

Fredrick alionyesha ustadi na kukipiga kikosi hicho jeki alipopiga ‘hat trick’. Nayo Migori Youth ilipata mabao yake kupitia Clinton Okoth na Konjestere Owenga.

”Ushindi huo utapata wachezaji wangu motisha zaidi na kujituma kwenye mechi sijazo,” kocha huyo wa Shabana alisema na kuongeza kuwa analenga kumaliza kati ya kumi bora ndani ya mechi za mkumbo wa kwanza.

Ushuru ya kocha, James ‘Odijo’ Omondi ilishuka na kutua saba bora kwa alama 27, moja mbele ya Mt Kenya United iliyotoka mabao 2-2 na Vihiga Bullets.

Nayo FC Talanta ilichomwa 3-0 na Kibera Black Stars, APs Bomet ilidungwa 3-1 na Coast Stima, St Josephs Youth ilitoka 3-3 na Murang’a Seal huku Fortune Sacco ikizoa 3-1 dhidi ya Vihiga United.