Michezo

City Stars njiani kurejea Ligi Kuu baada ya kufana

March 17th, 2020 2 min read

GEOFFREY ANENE na VICTOR OTIENO

NAIROBI City Stars imejawa matumaini kuwa itarejea kwenye Ligi Kuu ya Kenya msimu ujao baada ya kuzima Nairobi Stima 1-0 wikendi na kufungua mwanya wa alama 10 juu ya jedwali la Ligi ya Supa.

Zikisalia mechi 10 ligi ya daraja ya pili inayodhaminiwa na kampuni ya kamari ya Betika, City Stars, ambayo ilishushwa ngazi kutoka Ligi Kuu mwaka 2016, inaongoza kwa alama 64 kutokana na mechi 26 kwenye ligi hiyo ya timu 19.

Baada ya kuzamisha Stima uwanjani Camp Toyoyo jijini Nairobi, kocha Sanjin Alagic sasa anaamini hakuna kitu kiitakachozuia vijana wake wa City Stars kuingia Ligi Kuu.

“Lengo langu kutoka msimu uanze lilikuwa kutamatisha ligi katika nafasi mbili za kwanza. Ushindi huu ulikuwa muhimu sana katika kutimiza lengo hili na ninaamini kuwa tuko asilimia 99.9 ndani ya Ligi Kuu. Sioni timu inayoweza kuziba mwanya ambao tumefungua,” alisema Alagic akiwa amejawa na furaha. Vijana wake walikung’uta Stima 2-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza.

Katika mechi 26 ambazo zimesakatwa, City Stars imezoa ushindi mara 20, kutoka sare nne na kupoteza mbili pekee.

Ufanisi huo umefanya vijana wa Alagic kuwa juu ya nambari mbili Bidco United kwa alama 10. Bidco ilitarajiwa kucheza mechi yake ya 27 wikendi iliyopita dhidi ya Fortune Sacco, lakini mechi hiyo haikuchezwa mjini Kirinyaga kwa sababu ya hofu ya maambukizi ya virusi vya corona.

Kichapo cha Nairobi Stima kimetonesha kidonda cha klabu hiyo ambayo sasa imeanza kuonekana itakosa tiketi ya kupandishwa daraja baada ya kupoteza pembamba msimu uliopita.

Wanaumeme wa Nairobi Stima wameteremka nafasi moja hadi nambari tano. Wamezoa alama 48, pointi nne nyuma ya nambari tatu Vihiga United nayo Coast Stima ni ya nne kwa alama 49. Coast iliruka wanaumeme hao wenzao baada ya kuchabanga Polisi wa Utawala (AP) 3-1.

Licha ya kuteleza, kocha wa Nairobi Stima Leonard Odipo amesisitiza kuwa bado vijana wake hawajaaga mbio za kushiriki Ligi Kuu. Aidha, alisema masaibu yao yamechangiwa pakubwa na usimamizi mbovu wa marefa uwanjani.

“Nahisi hatujapoteza mechi kihalali. Hiki si kisa cha kwanza. Tumelalamika hapo awali na sasa inafaa watu husika kuchukua hatua,” alisema Odipo. Aliongeza, “Bado hatujasalimu amri ya kuwania tiketi ya kuingia Ligi Kuu. Tutashinda mechi zetu.”

Vihiga United ilibwaga Shabana 3-1. Shabana ni ya 10 kwa alama 35 nayo APS Bomet inasalia katika mduara hatari wa kuangukiwa na shoka baada ya kulimwa 1-0 na Murang’a Seal inayopatikana katika nafasi ya 11.

Modern Coast Rangers ilizaba Kenya Police 1-0 na kurukia nafasi ya 14 baada ya kusukuma FC Talanta nafasi moja chini. Ligi hii, ambayo timu za kwanza zitaingia Ligi Kuu moja kwa moja na pia nambari tatu ikipiga nambari 15 kutoka Ligi Kuu, imeenda mapumziko ya lazima kwa sababu ya mkurupuko wa virusi vya corona.