Michezo

City Stars wafichua malengo yao baada ya kumtwaa beki Kennedy Ouma Onyango kutoka Kakamega Homeboyz

October 24th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BEKI Kennedy ‘Vidic’ Ouma Onyango ameingia katika sajili rasmi ya Nairobi City Stars kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kuagana na kikosi cha Kakamega Homeboyz.

Nyota huyo kwa sasa atalazimika kukabili ushindani mkali kutoka kwa Edin Buliba, Wycliffe Otieni, Salim Abdalla na Mganda Yusuf Mukisa ili kupata nafasi ya kupangwa kwenye kikosi cha kwanza cha kikosi hicho kinachorejea kushiriki Ligi Kuu ya Kenya msimu huu.

“Nahisi kwamba nilifanya maamuzi bora ya kujiunga na City Stars. Hiki ni kikosi chenye malengo makubwa na kinachojivunia baadhi ya masogora wazoefu na wakufunzi wa haiba kubwa,” akasema Onyango.

Onyango alikuwa nguzo muhimu kambini mwa Homeboyz katika msimu wa 2019-20 uliomshuhudia akisakata jumla ya mechi 20 kati ya 22.

“Ujio wa Onyango ni afueni kubwa kwetu. Analeta tajriba pevu kambini mwa City Stars na atachangia pakubwa kuinua viwango vya ushindani,” akasema mratibu wa kikosi cha City Stars, Samson Otieno.

“Ni beki wa kutegemewa ambaye analeta nguvu mpya na uthabiti zaidi kwenye safu ya ulinzi. Hapana shaka kwamba kuwepo kwake kutaweka hai mengi ya maazimio yetu katika kampeni za mihula ijayo ligini,” akaongeza Otieno.

Onyango ndiye mwanasoka wa hivi karibuni zaidi kusajiliwa na City Stars baada ya Mukisa, Erick Ombija aliyetokea Gor Mahia na Sven Yidah aliyeagana na Kariobangi Sharks.

Hadi kusajiliwa kwa watatu hao, City Stars almaarufu ‘Simba wa Nairobi’, walikuwa pia wamejinasia huduma za wanasoka Rowland Makati kutoka Vapor Sports, Timothy Ouma (Laiser Hill Academy), Ronney Kola Oyaro (Kenya School of Government) na Elvis Ochieng Ochoro (Hakati Sportiff).

Wakati uo huo, kocha Sanjin Alagic wa City Stars amerejea humu nchini baada ya kuwa nje kwa likizo ya miezi saba. Mkufunzi huyo mzawa wa Bosnia alisafiri jijini Sarajevo mnamo Machi kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona.

“Najihisi vyema kurejea ugani baada ya kipindi kirefu bila. Sasa tunajiandaa kuanza mazoezi kwa minajili ya kampeni za msimu huu,” akasema Alagic

Kwa mujibu wa ratiba ya msimu ujao katika Ligi Kuu ya Kenya (FKFPL), City Stars wamepangiwa kufungua kampeni zao za 2020-21 dhidi ya Nzoia Sugar mnamo Novemba 22 kabla ya kuchuana na Zoo Kericho (Novemba 29).

Kikosi hicho kitapepetana baadaye na Homeboyz (Disemba 9), Western Stima (Disemba 13) na AFC Leopards (Disemba 19) kwa usanjari huo.

“Tuna furaha kurejea katika Ligi Kuu baada ya kuwa nje kwa misimu minne. Tunalenga kujifua vilivyo na kuchukulia kila mchuano kama fainali,” akatanguliza Alagic.

“Kubwa zaidi katika malengo yetu ni kufanya City Stars kuwa ngome ya wanasoka chipukizi watakaochangia vilivyo makuzi ya kabumbu ya humu nchini na watakaowaniwa na vikosi vya haiba kubwa ughaibuni,” akaongeza kocha huyo.