Michezo

City Stars wasajili wawili zaidi katika siku ya mwisho ya uhamisho wa wanasoka katika FKFPL

November 6th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Nairobi City Stars kimejinasia huduma za beki Herit Mungai Atariza na fowadi Rodgers Okumu kwa minajili ya kampeni za msimu ujao wa Ligi Kuu ya Kenya (FKFPL).

City Stars almaarufu ‘Simba wa Nairobi’ wamethibitisha kusajiliwa kwa wawili hao kutoka kambini mwa kikosi cha Coast Stima kinachoshiriki Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) na kukiri kwamba ujio wao unakamilisha kujishughulisha kwao katika soko la uhamisho wa wachezaji muhula huu.

Baada ya kurasimisha uhamisho wake hadi City Stars, Mungai ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Posta Rangers na Kariobangi Sharks alisema, “najihisi vizuri kusajiliwa na kikosi hiki ambacho nimekuwa na ndoto ya kukichezea.”

Okumu ambaye alikatiza uhusiano wake wa miaka mitano na Coast Stima, alifichua pia sababu za kujiunga kwake na City Stars.

“Napania kujikuza zaidi kitaaluma na kuwa sehemu ya kikosi hiki ambacho kinafahamika kwa upekee wa kuwapokeza wachezaji chipukizi malezi bora ya soka,” alisema kwa kuwaahidi mashabiki mambo makuu.

“Wakati wa mechi iliyotukutanisha na Coast Stima ugani Camp Toyoyo, Okumu aliridhisha sana. Alifunga bao na kuchangia mengine mawili. Hapo ndipo tulipoanza kuyawania maarifa yake,” akasema mratibu wa kikosi cha City Stars, Samsom Otieno.

City Stars wamejinasia pia huduma za wachezaji Ronney Kola Oyaro kutoka Kenya School of Government (KSG), Timothy Ouma wa Laiser Hill na kiungo wa Vapor Sports, Rowland Makati.

Mbali na hao, walijitwalia pia maarifa ya kipa wa Wazito FC, Steve Ngunge Ndungu na Elvis Ochoro aliyeagana rasmi na Hakati Sportif.

Mganda Yusuf Mukisa Lubowa (Proline FC) na Kennedy Onyango wa Kakamega Homeboyz ni miongoni mwa wachezaji wengine wapya waliosajiliwa na City Stars katika muhula huu wa uhamisho uliofungwa rasmi usiku wa Ijumaa ya Novemba 6, 2020.