Michezo

City Stars yaangusha APs Bomet BNSL

March 10th, 2020 1 min read

Na JOHN KIMWERE

WANASOKA wa Nairobi City Stars maarufu Simba wa Nairobi waliendelea kutetemesha wapinzani wao, kwenye kampeni za kuwania taji la Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL) baada ya kusajili mabao 2-1 dhidi ya APs Bomet uwanjani Green Stadium, Kericho.

Nayo timu ya Bidco United ilinyanyua Maafande wa Administration Police (AP) kwa mabao 2-1 na kuendelea kushikilia nafasi ya pili katika jedwali kwa kufikisha alama 54.

Naye mchana nyavu mahiri, Odhiambo Barrack alipiga kombora mbili safi na kubeba Ushuru FC kuadhibu Mt Kenya United kwa mabao 2-0 huku Migori Youth ikilimwa magoli 3-2 na Fortune Sacco.

City Stars ya kocha, Sanjin Alagin iliendelea kuhangaisha wapinzani wao kwenye kampeni za kufukuzia tikiti ya kufuzu kupandisha ngazi kushiriki Ligi Kuu msimu ujao.

City Stars ilipata mafanikio hayo baada ya Ezekiel Odera na Peter Opiyo kila mmoja kucheka na wavu mara moja.

Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Victor Ademba, Alex Imbusia na Dennis Wafula walitikisa wavu mara moja kila mmoja na kubeba Vihiga United kushinda vijana wa Kibera Black Stars (KBS) kwa mabao 3-0.

Nao wachezaji wa kikosi cha Coast Stima kilirejea makwao kwa tabasamu kiliandikisha ushindi wa mabao 2-1 mbele ya St Josephs Academy.

Kadhalika mchezaji shupavu, Ibrahim Elias aliachia kombora moja safi na kubeba FC Talanta kuangusha Nairobi Stima kwa bao 1-0.

Katika msimamo wa kinyang’anyiro hicho, City Stars ingali kidedea kwa kukusanya 61 baada ya kushuka dimbani mara 25.

Vihiga United ndio ya tatu kwa kutia kapuni pointi 49, moja mbele ya Nairobi Strima. Kwa kukusanya jumla ya alama 46, Coast Stima imefanikiwa kufunga tano bora baada ya kucheza mechi 26.