Michezo

City Stars yazidi kutetemesha Betika Supa Ligi

December 4th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE
TIMU ya Nairobi City Stars iliendelea kutesa wapinzani wengine kwenye kampeni za kufukuzia tajiu la  Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL)  baada ya kuchoma St Josephs Youth mabao 2-0 uwanjani Hope Center, Kawangware, Nairobi.
Nao vijana wa Vihiga United walilala kwa mabao 2-1 mbele ya Nairobi Stima uwanjani Mumias Complex mjini humo.
Ni bayana City Stars inazidi kuonyesha imepania kupambana mwanzo mwisho kutafuta tiketi ya kufuzu kushiriki Ligi Kuu ya KPL msimu ujao.
City Stars iliteremsha soka safi na kupata mabao hayo Davis Amuyunzu na Anthony Kimani waliofunga dakika ya 20 na 52 mtawalia. Ufanisi huo umefanya City Stars kushinda mechi 13 na kutoka nguvu sawa mara nne.
”Napongeza vijana wangu kwa kazi njema wanaendelea kufanya kwenye jitihada za kupigania tiketi ya kufuzu kupandishwa ngazi muhula ujao,” kocha wa City Stars, Sanjin Alagin alisema.
Hata hivyo alilaumu wachezaji wake kwa kutomakinika kwenye mchezo baada ya kupata nafasi nyingi wangevuna ushindi mnono lakini walifanikiwa kupata mabao mawili.
Nayo APs Bomet ilipondwa magoli 3-2 na Bidco United ya tatu kwenye jedwali kwa alama 32 sawa na Vihiga United.
Bidco ilibeba ufanisi huo pale Jacob Onyango alipocheka na wavu mara mbili huku Eric Gichimu akitiingia goli moja. Nao Brian Ngala na Simon Karanja wa APs Bomet kila mmoja alitikisa wavu mara moja.
Kwenye mechi hizo, Fortune Sacco ilipigwa 1-0, MKU ilibamiza Shabana 3-1, Kenya Police ilidhalilishwa kwa magoli 7-0 na Coast Stima, Murang’a Seal iliranda Modern Coast Rangers 3-1 huku Migori Youth ikitoka sare tasa na Kibera Blackstars.
City Stars ina alama 43, sita mbele ya Nairobi Stima nayo Bidco United inafunga tatu bora.