City Stars yazidi kutetemesha kipute cha BNSL

City Stars yazidi kutetemesha kipute cha BNSL

Na JOHN KIMWERE

KIKOSI cha Nairobi City Stars maarufu Simba wa Nairobi kiliendelea kutesa kwenye kampeni za taji la Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL) kilipochoma Maafande wa Kenya Police mabao 2-1 uwanjani Hope Center, Kawangware Nairobi.

Nayo Bidco United iliona giza iliponyukwa magoli 3-0 na St Joseph Youth Academy huku Coast Stima ikibugiza majirani zao Modern Coast Rangers mabao 3-0.

City Stars ya kocha, Sanjin Alagin ilijitahidi kiume na kuweka pengo la alama saba dhidi ya wapinzani wao karibu Bidco United.

Wanasoka hao waliopania kujiongezea tumaini la kusonga mbele kwenye kampeni za kipute cha msimu huu walizoa ufanisi huo kupitia Ezekiel Odera na Peter Opiyo waliotikisa wavu mara moja kila mmoja.

Meneja wa City Stars, Neville Pudo alisema ”Bila shaka tunashukuru wachezaji wetu kwa kuendelea kuonyesha wamepania kutwaa tikiti ya kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu ya KPL muhula ujao.”

Nao wachana nyavu Eric Ombija, Rodgers Okumu na Khamis Abudu walifungia Coast Stima bao moja kila mmoja na kuzima ndoto ya majirani zao ya kusajili alama tatu muhimu.

Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Alex Imbusia na Dennis Wafula kila mmoja alitikisa wavu mara moja na kubeba Vihiga United kuangusha Maafande wa Administration Police (AP) kwa kuidunga mabao 2-0 huku Nairobi Stima ikilimwa bao 1-0 na Migori Youth kupitia Mark Ochieng alipofunga dakika ya 50.

Kwenye kampeni za ngarambe hiyo, Mt Kenya United ilizabwa mabao 3-1 na Fortune Sacco, FC Talanta iliuma APs Bomet kwa mabao 2-1, Vihiga Bullets ilicharaza Kibera Black Stars mabao 2-0.

  • Tags

You can share this post!

Haji, Kinoti wakana madai kuwa wamekosana

RIZIKI: Habagui kazi licha ya kuwa mhitimu

adminleo