CLARA VUGUTSA: Nalenga kuwapa mafunzo ya uigizaji wasanii chipukizi

CLARA VUGUTSA: Nalenga kuwapa mafunzo ya uigizaji wasanii chipukizi

Na JOHN KIMWERE

NI miongoni mwa wasanii wa kike wanaoibukia wanaolenga kusaidia wenzao na kupiga hatua katika tasnia ya maigizo miaka ijayo. Ni taaluma aliyoiwazia tangia akiwa mdogo akisoma katika Shule ya Msingi ya Kwa Njenga, Mukuru, Nairobi. Hata hivyo alipoteza imani kabla ya kufanya mtihani wa darasa la nane.

Kando na uigizaji anasomea masuala ya stima kwenye Taasisi ya Kenyan Christian Industrial Training Institute (KCITI). Pia ni muokaji wa mikate na mfanyi kazi wa kujitolea kwa jamii katika masuala ya afya.

Clara Nyaligu Vugutsa almaarufu Kasy ameorodheshwa kati ya waigizaji wanaolenga kufanya kweli katika jukwaa la burudani nchini.

Licha ya kushiriki filamu ya ‘Hulabaloo Eastate’ iliyopeperushwa kupitia runinga ya Maisha Magic ameibuka kati ya wanamaigizo wanaoshiriki filamu nyingine inayozidi kuzua gumzo kibao katika mitandao ya kijamii. Filamu hiyo inayokwenda kwa jina ‘Vituko mitaani’ inaoneshwa kuipitia runinga ya mtandaoni inayokwenda kwa jina Hollywave TV.

”Ingawa nilikuwa nimepoteza imani na masuala ya maigizo nilianza kuwazia tena mwaka 2015 nilipojiunga na kundi la Hollywave wakati huo nikisoma kidato cha tatu kwenye Shule ya Nileroad Nairobi,” alisema na kuongeza kwamba bado “sijayeyusha matamanio ya kufanya vizuri katika sekta ya uigizaji.”

Dada huyu mwenye umri wa miaka 23 anasisitiza kuwa ana talanta ya uigizaji ambapo ingawa nia yao sio umaarufu anataka kushiriki filamu na zifanikiwe kuoneshwa kupitia runinga mbali mbali nchini.

Kando na filamu hizo pia anajivunia kufanya kazi nyingine kama Talanta Mtaani 2017.

Binti huyu mwenye tabasamu ya kuvutia anasema analenga kufuata nyayo za waigizaji wa kimataifa kama Terry Rothery (Canada) na Antonia Thomas (Uingereza). Wawili hao wanajivunia kushiriki filamu kama ‘Cedar Cove,’ ‘Christmas Getaway,’ na ‘Spike Island,’ ‘Firstborn,’ mtawalia.

Hata hivyo katika mpango mzima anasema analenga kuanzisha Taasisi ya kutoa mafunzo ya uigizaji wa wasanii chipukizi. ”Sio siri tena imegunduliwa kwamba wapo vijana wengi mitaani walituzwa kipaji cha uigizaji wanaohitaji kushikwa mikono ili kutimiza malengo yao,” akasema.

Kwa waigizaji wa kigeni anasema angependa kufanya kazi na wasanii kama Nadia Buari (Ghana) aliyeigiza filamu kama ‘Set apart,’ na ‘Darkness of Sorrow’ kati ya zingine. Pia yupo msanii wa filamu za Kinigeria (Nollywood) Eni Edo anayejivunia kushiriki kazi kama ‘ Only Love,’ na Chief Daddy’ miongoni mwa zingine.

Kwa waigizaji wa humu nchini anasema anatamani sana kufanya kazi na wenzake akiwamo Catherine Kamau ‘sue and Johny’ ‘Mother inlaw’ pia Sarah Hassan ‘Tahidi high,’ ‘Plan B.’

Kisura huyu ambaye akiwa mtoto akitamani kuhitimu katika taaluma ya uuguzi anatoa wito kwa serikali iwazie kutoa sapoti katika sekta ya uigizaji kama ilivyo katika kitengo cha spoti nchini. ”Serikali inahitaji kuwekeza vizuri katika tansia ya maigizo ili kuwafaidi wasanii wanaokuja wanawake na wanaume kwa jumla,” akasema.

You can share this post!

SALOME NJERI: Mtambue ‘Mama Chapo’ wa kipindi...

JOY KINYUA: Serikali ipige jeki uigizaji nchini