Habari

Cleophas Malala atupwa nje

June 26th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

BARAZA la uongozi la chama cha ANC limemfukuza Seneta wa Kaunti ya Kakamega Cleophas Malala kutoka chama hicho.

Hatua hiyo ambayo ilichukuliwa Ijumaa inajiri baada ya kamati ya nidhamu ya chama hicho Novemba 2019 kumuamuru Seneta huyo kufika mbele yake kujibu tuhuma za kukiharibia sifa chama hicho lakini akakataa.

Inadaiwa Bw Malala alitoa matamshi yaliyodunisha chama hicho na kiongozi wake Musalia Mudavadi wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mdogo katika eneobunge la Kibra, Nairobi mnamo Oktoba 2019.

“Matamshi yako na mienendo wakati wa mkutano wa kampeni ulioitishwa na ODM katika eneobunge la Kibra mnamo Oktoba 27, 2019, yalihujumu heshima na hadhi ya chama cha ANC, kiongozi wake, wanachama wake na wafanyakazi wake,” kamati hiyo ilisema na ikapendekeza Malala atimuliwe.

ANC pia inasema Bw Malala alikiuka Katiba yake na sheria ya vyama vya kisiasa (PPA) kwa kumpigia debe mgombeaji wa ODM katika uchaguzi mdogo wa Kibra Imran Okoth.

Hii ni licha ya kwamba chama hicho kilidhamini mtaalamu wa masuala ya uongozi Eliud Owalo, kama mgombeaji wake katika uchaguzi huo.