Habari Mseto

Co-op kuwapa wateja mikopo ya Sh2 milioni kwa simu bila mdhamini

August 25th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Benki ya Co-operative imesema kuwa itatoa mikopo isiyo na mdhamini hadi Sh2 milioni kwa biashara ndogo na za wastani.

Mikopo hiyo itatolewa kwa njia ya simu. Benki hiyo ilitangaza hilo baada ya kupokea mkopo wa Sh15.2 bilioni kutoka Shirika la International Finance Corporation (IFC) kutoa kwa biashara ndogo.

Mpango huo utasaidia sana wamiliki wa biashara ndogo kutokana na kuwa benki nyingi zimekoma kutoa mikopo kwa biashara hizo.

Hii ni kutokana na kuwekwa kwa viwango vya mwisho vya riba kwa mikopo na Benki Kuu baada ya sheria kupitishwa Septemba 2016.

Benki nyingi zilihofishwa na viwango hivyo, na kuzifanya kuacha kutoa mikopo ambayo haijadhaminiwa kwa sababu ya tishio la biashara nyingi kushindwa kulipa.

Benki hiyo itatoa mafunzo kwa wote watakaonufaika, alisema kaimu mkurugenzi wa biashara Arthur Muchangi, Alhamisi.