Habari Mseto

Co-op yasema serikali imeisaidia kuongeza kiwango cha faida

November 16th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Benki ya Cooperative imetangaza ongezeko la faida kwa asilimia nane baada ya kutozwa ushuru katika muda wa miezi tisa ya mwanza mwaka huu, kufikia Septemba.

Ukuaji wa faida umefanikishwa na mapato yaliyoimarika kutokana na riba inayotozwa dhamana za serikali na upungufu wa mikopo ambayo haifanyi vyema, kulingana na benki hiyo.

Mapato ya Cooperative yaliongezeka hadi Sh10.31 bilioni kutoka Sh9.54 bilioni katika muda huo mwaka uliotangulia.

Pia, tawi lake la Sudan Kusini lilionekana kufanya vyema katika muda huo, ilisema benki hiyo katika taarifa.

Benki hiyo ilipata faida ya Sh235.12 milioni kabla ya kutozwa ushuru katika robo ya tatu ya 2018 ikilinganishwa na Sh39.15 milioni katika kipindi hicho 2017.

Mapato kutokana na dhamana za serikali yaliimarika kwa asilimia 13.5 kutoka Sh6.12 bilioni hadi Sh6.95 bilioni katika kipindi hicho.

Mapato kutokana na riba za mikopo yaliongezeka kwa asilimia moja hadi Sh23.77 bilioni kutoka Sh23.58 bilioni 2017.