Habari Mseto

Co-op yazoa faida ya Sh12.7 bilioni

March 21st, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Benki ya Co-operative imetangaza ongezeko la asilimia 11.6 la faida baada ya kutozwa ushuru hadi Sh12.7 bilioni kwa mwaka uliokamilika Desemba 2018.

Faida hiyo ilitokana na mapato kutokana na riba na kupungua kwa hasara inayotokana na mikopo kwa wateja.

Hasara ilipungua kwa nusu hadi Sh1.84 bilioni licha ya ongezeko la mikopo ambayo haikuwa inalipiwa kwa asilimia 56.7 au Sh10.6 bilioni hadi Sh29.4 bilioni.

Benki ya Cooperative ilirekodi ongezeko la asilimia 9.5 la mapato kutokana na riba hadi Sh30.8 bilioni, na kudhibiti hasara ya Sh600 milioni kutokana na mapato yasiyofadhiliwa ambayo yalikuwa ni Sh12.9 bilioni.

Upungufu katika mapato hayo ulitokana na ada iliyopungua kwa mikopo ya wateja kwa sababu ya benki kuongeza ufadhili wake kwa serikali na kupunguza mikopo yake kwa wateja.

Faida kutokana na dhamana kwa serikali iliongezeka kwa asilimia 16 au Sh11 bilioni hadi Sh80.24 bilioni mwaka huo huku kitabu chake cha mikopo kikipungua kwa Sh8.5 bilioni hadi Sh245.4 bilioni.

Kutokana na hilo, benki hiyo italipa washikadau wake mgao wa Sh1 kwa hisa ikilinganishwa na senti 80 zilizolipwa 2017.

Benki ya KCB pia imepata ongezeko la faida baada ya kutozwa ushuru kwa mwaka wa 2018 ambayo iliongezeka kwa asilimia 22 hadi Sh24 bilioni kutokana na kupunguza hasara katika mikopo na mapato kutokana riba ya juu ilhali mapato yasiyofadhiliwa hayakuongezeka au kupungua.