Michezo

Coast Stima yapoteza wasakataji wawili

June 18th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Coast Stima kinachoshiriki Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) kimepoteza huduma za wanasoka wawili, beki Idd Hassan na kiungo Dennis Magige, ambao wamerejea kambini mwa Bandari FC baada ya kipindi chao cha mkopo kukamilika.

Haya ni kwa mujibu wa kocha Paul Ogai ambaye amethibitisha kwamba mkufunzi Ken Odhiambo wa Bandari FC anahitaji huduma za wawili hao kwa minajili ya kampeni za kikosi chake msimu ujao.

Ingawa hivyo, kapteni Joshua Oyoo ambaye pia anachezea Coast Stima kwa mkopo kutok Bandari, atasalia kambini mwa kocha kocha Ogai anayejivunia pia maarifa ya Eric Ombija kwa mkopo kutoka kwa mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Gor Mahia.

Hadi alipopokezwa mikoba ya Coast Stima, Ogai alikuwa pia amewanoa wanasoka wa Kisumu All Stars, Western Stima katika KPL na kilichokuwa kikosi cha Palos FC.