Kimataifa

Coca-Cola kuanza kutengeneza soda yenye bangi

September 18th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

KAMPUNI ya kutengeneza vinywaji vya soda ya Coca-Cola imedokeza kuwa inawazia kuanza kutengeneza soda zilizo na chembechembe ya bangi ndani yake, wakati huu ambapo kampuni nyingi zimechangamkia soko la bangi.

Katika habari iliyotolewa Jumatatu, kampuni hiyo ilielezea wazo lake la kutaka kufanya hivyo,.

Kampuni hiyo, ilirejelea ripoti iliyotolewa na shirika la BNN Bloomberg ambayo ilisema ilikuwa kwenye mazungumzo na kampuni ya Aurora Cannabis Inc kutoka Canada ili kutengeneza vinywaji vilivyo na kemikali ya Cannabidiol (CBD) ambayo hutolewa ndani ya bangi na haina madhara.

Coke sasa inajiunga na kampuni zingine kubwa za pombe na sigara ulimwenguni ambazo zimelenga soko la bangi kabla ya kuzinduliwa rasmi kwa matumizi ya bangi kimatibabu nchini Canada, Oktoba 17.

Katika habari tofauti, Coke na Aurora zilisema zimependezwa na kutengeneza vinywaji vyenye chembechembe hizo zabangi, lakini hazingesema lolote kuhusu mambo haswa yaliyozungumziwa.

Vinywaji vyenye CBD sasa vitalenga kupunguza uchungu na mwili kuchoma, ripoti ya BNN ikasema.

Mchanganuzi kutoka Wells Fargo Bonnie Herzog alitaja habari hizo kuwa “za kufurahisha na zenye uwezo wa kuleta maendeleo” kwani zitapeleka Coke katika mazingira yatakayoisaidia kuimarisha afya.

Kuna uwezekano kuwa bidhaa zenye CBD zitakuwa tofauti na zile zinazotengenezwa na kampuni za pombe ambazo huenda zingewapa wanywaji kemikali iliyo ndani ya bangi inayochangamsha akili (THC).

Watengenezaji bia Constellation Brands, Molson Coors na Heineken’s Craft beer Laguinitas majuzi walianzisha bia aina ya Hi-Fi Hops ambayo ina ladha ya maji pamoja na kemikali za THC na CBD.

“Vinywaji vya THC huenda vinaenda vizuri na watengenezaji wa bia, na hivyo huenda CBD itaenda vyema na Coke, tukiangazia masuala ya kiafya,” akasema mchanganuzi kutoka Liberum, Nico Von Stackelberg.

Mchanganuzi mwingine kutoka Cowen, Vivien Azerutu alisema anatarajia kampuni nyingine kama PepsiCo kufuata mkondo huo.