‘Cohen alilazimika kumuoa Sarah ili asirudishwe kwao’

‘Cohen alilazimika kumuoa Sarah ili asirudishwe kwao’

NA RICHARD MUNGUTI

RAIA wa Uholanzi Tob Cohen aliyeuawa na mwili wake kutupwa ndani ya shimo la choo alilazimishwa kufunga ndoa na Sarah Wairimu Kamotho ili asifukuzwe Kenya, mahakama kuu ilifahamishwa Jumatatu.

Jaji Murungi Thande anayesikiliza kesi ya kupinga Wosia wa kugawa mali alioandika Cohen alifahamishwa kuwa marehemu alishurutishwa kumuoa Sarah ili asitimuliwe Kenya.

Akitoa ushahidi mbele ya Jaji Thande, Bi Gabrielle Hannahn Van Straten alisema ndugu yake alimpelekea ujumbe wa barua pepe na kumweleza “endapo Sarah ataniua uchukue mali yangu.”

Katika ushahidi aliotoa mbele ya Jaji Thande, Gabrielle alisema Wosia wa Cohen uliotayarishwa na kuhifadhiwa na wakili Chege Kirundi ulifafanua kwa urefu jinsi mali yake itagawanywa.

“Ndugu yangu alisema katika wosia uliosomwa na Bw Kirundi nipewe nusu ya mali yake kisha asilimia 25 ipewe wapwa zake – Seth na Sharon,” Gabrielle alimweleza Jaji Thande.

“Je katika wosia huo ulisikia jina la Sarah Wairimu Kamotho likitajwa,” wakili Danstan Omari anayewakilisha familia ya marehemu aliuliza.

“Hapana, jina la Sarah Wairimu Kamotho halikutajwa. Hakugawiwa chochote,” alijibu Gabrielle.

Mahakama ilielezwa kwamba baada ya Wosia huo kufunguliwa na kusomwa mbele ya watu 24 miongoni mwao aliyekuwa Waziri Msaidizi Patrick Muiruri alirudi Uholanzi kuhudhuria harusi ya mwanawe na hakusubiri mazishi ya nduguye.

Dadaye marehemu alikana madai kuwa “hakuhudhuria mazishi ya ndugu yake kwa vile alichokuwa akitaka tu ni mali.”

Alisema wakati mazishi ya Cohen yakifanyika, Sarah alikuwa amekamatwa kushtakiwa kwa mauaji ya mumewe na kuzuiliwa katika gereza la wanawake la Lang’ata kaunti ya Nairobi.

Hata hivyo, Sarah alisindikizwa na askari jela kuhudhuria mazishi ya Cohen.

Gabrielle alisema ndoa kati ya nduguye marehemu na Sarah Wairimu haikuwa ya hiari.

“Ndugu yangu alishurutishwa kufunga ndoa na Sarah na familia yake (Wairimu) ili asifukuzwe Kenya,” Gabrielle alieleza Jaji Thande.

Akiongozwa kutoa ushahidi na wakili Danstan Omari, Gabrielle alisema mbali na Sarah, nduguye alikuwa amefunga ndoa na wanawake wengine wawili hapo awali.

“Mbali na Sarah nduguyo alikuwa amefunga ndoa na wanawake wengine,” Bw Omari alimwuliza Gabrielle.

“Ndio alikuwa amefunga ndoa na wanawake wengine wawili raia wa Uholanzi lakini hakuwa amepata watoto nao,” alijibu Gabrielle.

Alieza korti Tob alikuwa amehasiwa na kwamba hakuwa na uwezo wa kupata watoto.

“Akiwa na umri wa miaka 27 ndugu yangu alihasiwa kwa hiari yake na hivyo hakuwa na uwezo wa kuwapata watoto,” Gabrielle alitoboa siri ya nduguye.

Kesi inaendelea kusikilizwa.

  • Tags

You can share this post!

Nambari ya simu ‘ya Ruto’ yamulikwa ICC

Digrii: Afueni kwa Jumwa korti ikikataa ombi la kumzuia...

T L