Commandos waaibishwa na Shabana FC katika NSL

Commandos waaibishwa na Shabana FC katika NSL

Na CECIL ODONGO

SHABANA FC, wikendi ilivuna ushindi mkubwa wa 7-2 dhidi ya Green Commandos ya Kakamega ugani Gusii, katika raundi ya 15 ya mechi za Ligi ya Supa nchini (NSL).

Mshambulizi Ekaliani Ndolo aliibuka shujaa katika mechi hiyo baada ya kufunga mabao matatu huku Dennis Onyancha akifunga mawili nao Bob Mugalia na Daniel Murage wakafunga bao moja kila moja. Mabao mawili ya Green Commandoes yalifungwa na Bernard Awathi na Lihanga Castro.

Ushindi huo uliwapaisha vijana wa kocha Gilbert Selebwa hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa jedwali la NSL kwa alama 22 nao Green Commandos wakisalia katika nafasi hatari ya 19 mkiani mwa jedwali hilo.

Naibu kocha wa Shabana FC Andrew Kanuli aliyesimamia mechi hiyo kutokana na marufuku anyaotumikia Selebwa, aliwasifu vijana wake kwa kujiinua na kutwaa ushindi huo haswa baada ya kichapo cha katikati ya wiki jana dhidi ya Fortune Sacco.

Katika mechi nyingine, FC Talanta iliichapa Kangemi Youth 2-0 na kupunguza mwanya wa alama unaotamalaki kati yake na viongozi wa ligi ,Wazito FC hadi alama tatu. Rodgers Omondi na Anthony Gichu waliandikisha mabao yote kwa washindi ugani Camp Toyo.

Ushuru FC nao walikosa kutumia uga wao wa nyumbani wa Ruaraka ili kuondoa Wazito FC kileleni mwa ligi hiyo kwa kukubali sare ya 1-1 dhidi ya wageni wao, Coast Stima.

Nairobi Stima walitwaa ushindi wa 1-0 dhidi ya Migori Youth uwanjani Karuturi, Naivasha kusalia katika nafasi ya tatu ligini nao Eldoret Youth ikaagana sare tasa na Fortune Sacco.

You can share this post!

Mudavadi atoa wito Serikali isaidie wachezaji wakongwe

MAPOZI: Mwanamuziki Evelyne Wanjiru

adminleo