Michezo

Conte akiri Chelsea kuingia Nne Bora ni ndoto

April 8th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa Chelsea, Antonio Conte amehisi kuwa sare ya 1-1 dhidi ya West Ham Jumapili nyumbani Stamford Bridge ndiyo kilele cha masaibu ya timu yake msimu huu.

Licha ya kumiliki mpira, Chelsea haiuwa na cha kujivunia ila bao moja lililofungwa na Cesar Azpilicueta, mengine yote yalikuwa mabao hewa.

Straika aliyenunuliwa kutoka Real Madrid, Alvaro Morata alitamauka wakati mabao yake mawili walitupiliwa mbali kwa kuotea huku kipa wa West Ham, Joe Hart akionyesha sababu ya kutong’olewa michumani katika timu ya taifa ya Uingereza.

Na baada ya dakika tatu tu za kipindi cha pili, nguvu mpya  Javier Hernandez alisawazisha baada ya kupata krosi ndani ya kijisanduku cha Chelsea na kuipa West Ham ponti moja.

Mabingwa hao watetezi sasa wako nyuma kwa pointi 10 kufikia nambari 4 Tottenham huku Conte akikiri kuwa kuingia nne bora sasa ni ndoto.

“Lazima tumakinike. Lazima ushinde mechi hii ikiwa unalenga kusonga mbele. Hapa lengo ni kupata nafasi ya kucheza kwa Klabu Bingwa Ulaya, Uefa. Msimu huu tumehangaika sana, lakini mchuano huu unaeleza zaidi masaibu yetu. Katika mechi nyingi unaweza kuunda nafasi za kufunga, lakini kama hufungi mabao….,” akasema baada ya mechi.

“Ni mara ngapi nimesema hatukutumia vema nafasi zetu? Mara nyingi, na sasa kwa nafasi moja, tunapigwa bao.”