Michezo

Conte asema kila mtu Chelsea abebe lawama

February 12th, 2018 2 min read

Wachezaji wa Chelsea waondoka uwanjani baada ya kupewa kichapo cha 4-1 na Watford. Picha/ Hisani

LONDON, UINGEREZA

Na MASHIRIKA

Kwa Muhtasari:

  • Conte asema wadau wote wa Chelsea wafaa kulaumiwa kwa mtokeo duni 
  • Chelsea ilipewa kichapo cha 3-0 na Bournemouth baada ya adhabu ya 4-1 na Watford
  • Vijana wa Conte wameratibiwa kuchuana na Barcelona uwanjani Stamford Bridge, kabla ya Chelsea kusafiri ugani Old Trafford kuvaana na Manchester United, kisha kuwa wageni wa Manchester City 

KOCHA Antonio Conte wa Chelsea amesema kwamba wadau wote kambini mwa kikosi hicho wanastahili sehemu ya lawama anayoelekezewa kwa sasa kutokana na matokeo duni ambayo mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wamesajili kufikia sasa msimu huu.

Ingawa Chelsea walitarajiwa kutetea kwa mafanikio ufalme wa EPL waliolitia kapuni msimu jana chini ya Conte aliyekuwa akihudumu uwanjani Stamford Bridge kwa mar ya kwanza, miamba hao wa Uingereza wamesuasua mno na kuonekana wanyonge machoni pa wapinzani wao wakuu.

Kichapo cha 3-0 kutoka kwa Bournemouth na adhabu ya 4-1 ambayo Chelsea walipokezwa na Watford katika michuano miwili iliyopita ni matokeo ambayo yalitikisa pakubwa matumaini ya magwiji hao ya kutinga mduara wa nne-bora mwishoni mwa muhula huu na hivyo kuwa na hakika ya kunogesha kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

 

Lawama

Tangu kuwaongoza vijana wake kutia kapuni ubingwa wa EPL msimu jana, Conte amekuwa mwingi wa lawama kwa usimamizi wa Chelsea, akiwakosoa pakubwa kuhusu maamuzi ya kikosi hicho kutomhusisha kabisa katika shughuli za usajili wa masogora wapya waliojiunga na timu hiyo katika kipindi cha mihula iliyopita ya uhamisho wa wachezaji.

Isitoshe, kocha huyo wa zamani wa Juventus pia aliwashtumu vikali wachezaji wake kwa uoga walioudhihirisha uwanjani Vicarage Road ambapo walifungwa jumla ya mabao matatu chini ya dakika 10 za mwisho wa kipindi cha pili.

“Kikosi kinaposajili matokeo duni kama ambavyo Chelsea imekuwa ikifanya katika kipindi cha majuma kadhaa yaliyopita, muhimu zaidi ni kujisaka upya na kutathmini mchango wa kila idara na wadau mbalimbali,” akasema mkufunzi huyo mzawa wa Italia ambaye kwa mujibu wake, kushuka kwa kiwango cha ubora wa Chelsea kumechangiwa pakubwa na kutosajiliwa kwa wachezaji wa haiba kubwa muhula huu.

Baada ya kuvaana Jumapili na West Brom, Chelsea wamepangia kupepetana na Hull City katika mechi ya raundi ya tano ya Kombe la FA kisha kujipata katika ulazima wa kupiga michuano minne kwa mfululizo dhidi ya klabu tatu maarufu na za haiba kubwa. Kasyna stacjonarne w Polsce: https://kasynopl.com/kasyna-stacjonarne-w-polsce/

 

Mlima wa mechi

Chelsea wameratibiwa kuchuana na Barcelona uwanjani Stamford Bridge katika hatua ya 16-bora ya UEFA kabla ya Chelsea kusafiri ugani Old Trafford kuvaana na Manchester United kisha kuwa wageni wa Manchester City katika michuano ya haiba kubwa ya EPL.

Iwapo Conte atashindwa kuwatambisha Chelsea dhidi ya West Brom mnamo Jumatatu, huenda akajipata katika orodha ndefu ya makocha ambao wamefurushwa na mmiliki wa kikosi hicho, Roman Abramovich ambaye ana mazoea ya kuwafuta wakufunzi katikati ya misimu.

“Kibarua kilichopo mbele ya Chelsea si chepesi. Ugumu wa ratiba hiyo huenda ukaamua mustakabali wa Chelsea katika kampeni za msimu huu. Muhimu zaidi kwa sasa ni kumakinikia michuano ijayo na kutumainia kwamba wapinzani wetu watateleza na hivyo kutupa fursa ya kukamilisha kampeni kwa matao ya juu,” akasema beki na nahodha wa Chelsea, Gary Cahill.

Katika mojawapo ya mikakati ya kudumisha uhai wa matumaini yao katika kampeni za msimu huu, Conte amepania kubadilisha kikosi chake mara kwa mara kutegemea kiwango cha mchezo na uthabiti wa wapinzani wao.