Corona: Afrika Kusini sasa yadai ‘kuonewa’

Corona: Afrika Kusini sasa yadai ‘kuonewa’

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

Na MASHIRIKA

AFRIKA Kusini imedai kuwa inaonewa na mataifa mengine duniani badala kusifiwa, kwa kutambua aina mpya ya corona, inayoitwa Omicron.

Kwenye taarifa jana, Wizara ya Mashauri ya Kigeni nchini humo ilisema hatua ya baadhi ya mataifa kuwawekea masharti raia wake kusafiri huko ni ishara ya “adhabu” isiyofaa.

Tafiti za mwanzo ambazo zimetolewa na wataalamu zinaonyesha aina hiyo ya corona ni hatari na inasambaa kwa kasi.

Mnamo Ijumaa, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitaja aina hiyo ya corona kuwa “hatari.”

“Tunapaswa kupewa shukrani badala ya kuadhibiwa. Marufuku za usafiri ambazo zimetolewa ni sawa na kutuadhibu kutokana na hatua kubwa za kisayansi tulizopiga. Marufuku hizo zinasukumwa na siasa, wala si uhalisia wa kisayansi. Ni jambo lisilokubalika. Mbona Waafrika wanawekewa vikwazo kusafiri wakati virusi hivyo vimebainika katika mabara matatu?” ikashangaa wizara hiyo.

“Yanayoendelea kwa sasa ni mambo yasiyoepukika. Ni matokeo ya nchi nyingi kukosa kuwapa chanjo raia wake kwa njia inayofaa. Ni matokeo ya nchi zilizostawi kiuchumi kuficha baadhi ya chanjo hizo. Ni hali isiyokubalika hata kidogo,” akasema Ayoade Alakija, ambaye ndiye mwenyekiti mwenza wa kitengo cha Umoja wa Afrika (AU) kinachosimamia usambazaji wa chanjo hizo.

Visa kadhaa vimebainika barani Ulaya—viwili nchini Uingereza, viwili nchini Ujerumani, kimoja nchini Ubelgiji na kingine nchini Italia. Kisa kingine kimebainika katika Jamhuri ya Czech.

Mnamo Jumapili, Israeli ilianza kuwazuia raia wote wa kigeni dhidi ya kuingia nchini humo baada ya kubaini visa kadhaa vya virusi hivyo.

Kulingana na gazeti la ‘Times of Israel’, marufuku hiyo itatekelezwa kwa siku 14 zijazo.

Nchi nyingine ambazo zimebaini aina hiyo ya virusi ni Botswana na Hong Kong.

Nchini Uholanzi, mamia ya wasafiri wanaowasili huko kutoka Afrika Kusini wanafanyiwa ukaguzi kuhusu ikiwa wameambukizwa virusi hivyo.

Jumamosi, abiria 61 waliokuwa kwenye ndege mbili zilizotoka Afrika Kusini walibainika kuambukizwa.

Kulingana na maafisa wa serikali ya Uholanzi, abiria hao waliwekwa kwenye eneo lililotengwa karibu na Uwanja wa Ndege wa Schiphol.

Kwa sasa, Uholanzi ndilo taifa lililobaini visa vingi zaidi vya virusi hivyo baada ya Afrika Kusini.

Hapo jana, nchi hiyo ilianza kurejesha baadhi ya masharti yaliyokuwepo awali ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

Virusi hivyo vilibainika mara ya kwanza nchini Afrika Kusini Jumatano iliyopita.

Tayari, Uingereza imewapiga marufuku raia kutoka nchi za Afrika Kusini, Namimbia, Zimbabwe, Botswana, Angola, Msumbiji, Malawi, Zambia, Lesotho na Eswatini dhidi ya kuingia katika taifa hilo. Kulingana na masharti yaliyowekwa, watu pekee watakaoruhusiwa kuingia huko ni raia wa Uingereza au Ireland pekee.

Amerika pia imetoa masharti kama hayo. Serikali ya Amerika ilisema marufuku hiyo itaanza kutekelezwa leo.

Jumamosi, Australia ilisema itapiga marufuku safari za ndege kutoka mataifa hayo kwa siki 14 zijazo.

Raia wa Australia ambao wamekuwa katika nchi hizo kwa siku 14 zilizopita wamepigwa marufuku dhidi ya kusafiri nchini humo.

Japan ilisema wasafiri kutoka mataifa ya Kusini mwa Afrika watalazimika kukaa karantini kwa siku 10 kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini humo.

India nayo imewaagiza maafisa wake kuwakagua vikali watu wanaosafiri kutoka Afrika Kusini, Botswana na Hong Kong ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

You can share this post!

Mazungumzo ya ushirikiano wa kisiasa ni jambo la kawaida...

TALANTA YANGU: Kiongozi wa maskauti

T L