Habari Mseto

CORONA: Aibu ya Naibu Gavana kukataa kujitenga

March 22nd, 2020 1 min read

Na CHARLES LWANGA

HOFU ya kuambukizwa virusi vya corona imetanda katika Kaunti ya Kilifi baada Naibu Gavana Gideon Saburi, ambaye alikuwa amesafiri Ujerumani, kutangamana na wakazi kwenye hafla mbalimbali badala ya kujitenga kwa siku 14.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, jana alisema Bw Saburi ametengwa kwa lazima na atawekwa katika wadi ya kibinafsi hospitalini kwa siku 14, na atakapotoka atakamatwa na kushtakiwa.

“Afisa wa serikali Kilifi alikataa kujitenga. Tumemtenga kwa lazima kwa gharama yake mwenyewe na akimaliza muda tutamshtaki,’ akasema Bw Kagwe alipohutubia taifa jana jioni.

Wakazi wa Kilifi wamemkashifu Bw Saburi kwa kuhatarisha maisha ya wengi.

Wakazi walilalamika kuwa Bw Saburi baada ya kurudi nchini alianza kuhudhuria vikao vya umma badala ya kujitenga jinsi ilivyoagizwa na serikali.

Kulingana na baadhi ya ripoti, naibu gavana huyo ambaye alirudi kutoka Ujerumabi mnamo Machi 8, alihudhuria mkutano wa wafanyikazi wa kaunti, baraza la mawaziri na mkutano wa umma kabla ya kujitenga kwa 14 kulingana na maagizo.

Lakini kulingana na Mbunge wa Kilifi Kusini Ken Chonga, naibu huyo wa gavana alimwambia kuwa baada ya kurudi nchini alijipeleka katika hospitali ya Mombasa ambako alilazwa kwa siku tatu.

“Aliniambia madaktari walimchunguza na kumwachilia kwenda nyumbani baada ya kupata alikuwa mzima,” alisema Bw Chonga.

“Amesema hali yake ya afya ni njema, haugui na ana matumaini kuwa sampuli ambazo wamechukua kwa uchunguzi mara ya pili zitamwondolea lawama kuhusiana na hali yake ya afya,” akaongeza mbunge huyo.