Michezo

CORONA ARSENAL: Wachezaji watengwa

March 12th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

WACHEZAJI kadhaa wa Arsenal wametengwa baada ya kubainika kwamba mmiliki wa klabu ya Olympiakos, Evangelous Marinakis amepatikana kuwa na virusi vya Corona.

Kufuatia hatua hiyo, mechi ya EPL kati ya mabingwa watetezi Manchester City na Arsenal iliyopangiwa kuchezwa jana usiku ilifutuliwa mbali dakika za mwisho kama njia mojawapo ya tahadhari na kwa ugonjwa huo wa virusi hatari.

Arsenal ililazimika kufanya hivyo baada ya kubaninika kwamba Marinakis mwenye umri wa miaka 52, alikutana na baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo ya EPL ilipochuana na Olympiakos katika mechi ya Europa League mnamo Februari 27, 2020, ugani Emirates.

Marinakis ambaye pia ndiye mmiliki wa klabu ya Nottinghham Forest ya Uingereza, amekiri kwamba ameambukizwa virusi vya Corona.

Hata hivyo, Olympiakos itakutana na Wolves katika pambano jingine la Europa League baada ya UEFA kukataa ombi la Wolves kutaka mechi hiyo ya raundi ya 16 bora iahirishwe.

Kadhalika wasimamizi wa mechi za EPL wamesema hawana mpango wowote wa kuahirisha mechi zao, baada ya kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba hatua zifaazo zimechukuliwa.

Kutokana na msimamo huo, mechi kati ya Brighton na Arsenal itachezwa Jumamosi kama ilivyopangwa.

Kulingana na utafiti wa kina, ugonjwa huu ulioanzia nchini China haujapenyeza sana nchini Uingereza, ingawa kuna ripoti kwamba kuna waathiriwa wachache kufikia sasa.

Kufikia jana kulikuwa na ripoti kwamba jumla ya watu 382 wameambukizwa virusi hiyo, huku sita wakipoteza maisha yao kutokana na maradhi hayo hatari.

Ugonjwa huo ambao unafanana na homa, huku mwathiriwa akikumbwa na matatizo ya kupumua, unasambaa kwa haraka ambapo kwa jumla watu 116,000 wameambukizwa.

Kwa jumla ugonjwa huu umevuruga shughuli za michezo nchini Italia ambapo chama cha soka kimeamuru mechi zote za Serie A zichezwe pasipowepo mashabiki uwanjani. Ndivyo hali ilivyo pia nchini Ufaransa.

Mechi za Klabu Bingwa zinazohusu timu za Manchester United, Rangers na Chelsea, kadhalika zitachezwa bila mashabiki kuhudhuria.

Hali hii imevuruga mpango wa Liverpool kutwaa ubingwa wa EPL mwishoni mwa juma hili kama ilivyobashiriwa.

Vigogo hao wangetwaa ubingwa huo mwishoni mwa juma hili kama Arsenal ingeichapa City ugani Etihad, nao waibuke na ushindi dhidi ya Burnley.

Arsenal imesema wachezaji kadhaa- ambao klabu hiyo haikutaka kutaja walikutana na bwanyenye Marinakis, mara tu baada ya mechi yao na Olympiakos kumalizika.

“Habari zinasema kwamba wachezaji hao wanaweza kushikwa na ugonjwa huo wakati wowote, na kwamba inabidi watengwe kwa siku 14 tangu wakutane na tajiri huyo.

Kutokana na sababu hiyo, wachezaji hao hawangecheza jana usiku dhidi ya Manchestyer City, na EPL imeamua mechi hiyo isukumwe mbele.

Wachezaji hao watabakia manyumbani mwao hadi siku 14 zimalizike. Maafisa wao walioketi karibu na Marinakis wakati wa mechi hiyo, kadhalika watabakia manyumbani mwao hadi siku hizo ziishe kesho.