Makala

CORONA: Changamoto za kununua bidhaa dukani kwa njia za kidijitali

March 23rd, 2020 2 min read

 

Na GEOFFREY ANENE

Wanunuzi wanaotumia huduma ya kulipia bidhaa kwa kutumia simu wanapitia changamoto jinsi mwandishi huyu alipata kufahamu alipozuru maduka kadhaa.

Huduma hiyo imependekezwa na Rais Uhuru Kenyatta ili kuzuia uenezaji wa virusi hatari vya corona kupitia malipo ya pesa taslim.

Katika duka la kwanza, niliitisha pakiti moja ya unga wa ugali (Sh130) na sukari kilo moja (Sh120) hapo Machi 20 jioni. Nilipoambia muuzaji kuwa namtumia Sh250, alicheka tu na kusema ‘sawa’.

Sikupata tatizo kujaza gesi ya mtungi mdogo katika duka lingine siku hiyo, ambao hata hivyo, bei yake imepanda kutoka Sh800 miezi miwili iliyopita hadi kati ya Sh1,000 na Sh1,100 mtaani Kariobangi South Civil Servants.

Nilirudi kwenye duka la kwanza siku ya pili kununua staftahi. Niliitisha mkate wa gramu 400, ambao bei huwa Sh50, na maziwa ya Sh50.

Niliposema nalipa kwa kumtumia fedha, muuzaji alisema, “Aiii! Tena unalipa kwa kutumia simu? Huu ni mchezo sasa umeanza… Unanitumia Sh100 ya bidhaa hizi ama unaongeza kitu juu ya hizi fedha?” aliuliza akiwa amevalia sura ambayo ilionyesha hakufurahia kulipwa kwa njia hiyo na kama ni kulipa njia hiyo, fedha zinastahili kuwa juu kuliko anayelipa pesa taslim.

Hata hivyo, alikubali nimtumie Sh100 ya bidhaa hizo, japo shingo upande.

Siku ya tatu, mwandishi huyu aliamua kujaribu duka tofauti akitafuta kiamshakinywa. Aliitisha mkate (Sh50) na maziwa (Sh25) na kuongeza dawa ya sugua meno ya Colgate Herbal (Sh50). Ilipofika wakati wa kulipa, niliitisha nambari ya simu ya muuzaji ili nilipe Sh150. Kwa mshangao, muuzaji alisema “Sina simu” kabla ya kuongeza, “hapa tunauza bidhaa cash (pesa taslim).”

Kwa sasabu sikuwa na pesa taslim, nilielekea katika duka lingine, ambalo muuzaji hakuwa na tatizo na niliponunua mkate na dawa ya kupiga mswaki. Hata hivyo, nilikumbuka nimesahau maziwa na nikaingia katika duka tofauti. Habari ya asubuhi? Nataka uniuzie maziwa pakiti kubwa (Sh50)? Nilisema.

Nilipoletewa na kusema namtumia fedha kwa simu yake alisema, “Pole…Mimi nimetumia huduma ya Fuliza.”

Fuliza ni aina ya mkopo kutoka kwa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom, ambayo mtu anakopa kwa kutumia mtu mwingine fedha licha ya kuwa hana chochote kwenye simu yake ama anatuma kiasi ambacho kinazidi fedha alizonazo kwenye simu.

Mkopo huo unalipwa mara tu mkopaji anatumiwa ama kuweka fedha kwenye akaunti yake ya M-Pesa.

Wauzaji wengine wanasema simu zao hazina moto wakitaka kulipwa kwa noti.

Mkurupuko wa virusi vya corona ulianzia mjini Wuhan zaidi ya miezi miwili iliyopita na kuenea dunia nzima kwa haraka.

Kufikia Jumapili asubuhi, watu 308, 535 walikuwa wamethibitishwa kuwa na virusi hivyo duniani, huku 13, 069 wakiaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi hivyo. Kenya imethibitisha kesi saba za virusi hivyo katika mipaka yake.

Baadhi ya hatua Kenya imechukua kupunguza maambukizi ni kufunga taasisi za elimu, kushauri watu kuepuka mikusanyiko mikubwa, kunawa kila mara kwa kutumia ‘sanitizer’, kupunguza idadi ya watu wanaoabiri magari na treni na kutuma fedha kulipia huduma badala ya pesa taslim.