Habari MsetoSiasa

CORONA: Gavana azima watu kwenda Murang’a

March 26th, 2020 1 min read

PHYLLIS MUSASIA Na Alex NJERU

GAVANA wa Murang’a Mwangi Wa Iria amepiga marufuku shughuli zote za usafiri wa umma katika kaunti yake, huku bodaboda wakikatazwa kuhudumu Nakuru.

“Hatuwezi kusafisha maeneo ya steji kila siku na pia turuhusu watu waendeshe shughuli zao huku,” akasema Bw Iria.

Hata ingawa serikali imepunguza idadi ya wasafiri kwenye magari, Bw Iria alisema hilo pekee haliwezi kuzuia maambukizi ya virusi vya corona katika sekta ya usafiri.

Alisema polisi watatumwa katika steji zote za kaunti hiyo ili watu wote ambao wanataka kusafiri waeleze sababu zao.

“Watu walio na shida za magonjwa kama vile ya kisukari au figo, watatibiwa katika hospitali za hapa. Hatutawarusu kusafiri,” akaongeza.

Hatua hiyo ilisababisha matatizo makubwa kwa wananchi waliokuwa wakisafiri kuelekea na kutoka Murang’a jana.

Nako Nakuru, Mratibu wa Bonde la Ufa, Bw George aliwataka wakazi wajihadhari na matumizi ya bodaboda na badala yake watembee kwa miguu wanapoingia mjini.

Steji zote za magari zimehamishwa hadi nje ya mji wa Nakuru, na sasa magari yanayoelekea Nairobi na Nyahururu, yatabeba na kushukisha wateja katika uwanja wa Ziwani karibu na kanisa la Kingdom Seekers.

Magari yanayoelekea Magharibi mwa nchi, Eldoret, Kericho na Mogotio, yatatakiwa kufanyia kazi katika eneo la Railways karibu na sehemu maalumu ya ukaguzi wa magari.

Na Katika kaunti ya Meru, magari yote ya kampuni ya Meru Nissan Sacco yamesimamisha safari zote ili kukabili maambukizi ya corona.Magari hayo ambayo husafiri kutoka Meru-Nairobi na Nairobi-Mombasa, yamesitisha safari kuanzia hivi leo.

Akiongea na wanahabari mjini Chuka, mwenyekiti Wanja Karuku alisema jumla ya magari 680 hayatafanya kazi hadi itakapotangazwa tena.

Zaidi ya wafanyikazi 3,000 wakiwemo madereva, makanga, wahudumu wa vituo vya mafuta na wale wa ofisini wametumwa katika likizo ya lazima hadi hapo baadaye.