Habari

CORONA: Hakuna kwenda kanisani, msikitini

March 19th, 2020 2 min read

Na PHYLLIS MUSASIA

BAADHI ya makanisa na misikiti imetangaza kusitisha ibada pamoja na shughuli nyinginezo ili kuwakinga waumini kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona. Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Jackson Ole Sapit, alitangaza kusitishwa kwa huduma zote za kanisa ikiwemo ibada za Jumapili, sherehe za harusi na mazishi.

Kwenye taarifa yake, Askofu Sapit aliwataka waumini wote kuomba wakiwa nyumbani na familia zao na kuhakikisha kwamba wanajitenga na makundi ya idadi kubwa ya watu.

Kuhusu sakramenti takatifu, askofu Sapit alisema shughuli hiyo itafanywa kwa utaratibu spesheli utakaotolewa.

Waumini watatakiwa kushiriki ibada na maombi kupitia njia ya teknolojia. Ibada zitapeperushwa moja kwa moja kwenye mitandao kama vile Facebook na tovuti rasmi za kanisa hilo.

“Kila Jumapili kutakuwa na matangazo ya moja kwa moja kuanzia saa mbili asubuhi na Jumatano saa kumi na mbili jioni,” akasoma baadhi ya taarifa ya Askofu Sapit.

Kanisa hilo pia limeitaka serikali kuongeza juhudi za kukabiliana na janga hili kwa kuhakikisha wafanyakazi wote wanalindwa na waajiri wao.

Aidha, msikiti wa Jamia umetangaza kusitisha shughuli zake na ibada zote kwa waumini wake.

Katibu mkuu wa kamati ya msikiti huo Abdul Bary Hamid alisema kwenye taarifa kuwa hakutakuwa na mikutano yoyote ya maombi katika msikiti wa Jamia kwa muda usiojulikana.

Bw Hamid alisema uamuzi huo uliafikiwa baada ya mashauriano na baraza la Majlis Ulamaa na lile la wataalumu waislamu katika masuala ya matibabu (KAMMP).

“Tutazidi kufuatilia jinsi hali itakavyokuwa na kutoa taarifa zaidi kwa Waislamu wa Umma,” akasema.

Makanisa mengine yaliyofungwa ni Kanisa Katoliki la All Saints jijini Nairobi na makanisa yote ya Presbyterian (PCEA). Mikutano yote ya kanisa la PCEA imesitishwa kwa muda wa siku 21.

Ili kuendeleza shughuli za kanisa, wahubiri watatumia mitandao kuhubiri injili na kuombea jamii kwa jumla.

Wakati huo huo, jimbo kuu la Kanisa Katoliki, Nairobi limefutilia mbali ibada za Jumapili na hafla nyinginezo. Kwenye taarifa iliyotolewa Jumanne na kasisi Sammy Wainaina. Hata hivyo sehemu kuu ya maombi itabaki wazi kwa watu binafsi.

Wanaofanya usafi kanisani watahakikisha sakafu na sehemu zote zinasafishwa mara kadhaa kwa siku.

“Watakaofika kanisani kwa maombi binafsi watatakiwa kunawa mikono katika lango kuu na pia sehemu ya kufanya maombi kwa kutumia sabuni zilizowekwa katika sehemu hizo,” ikasema sehemu ya taarifa yake Kasisi Wainaina.

Yeyote atakayefika kanisani ametahadharishwa dhidi ya matumizi ya vitabu vya nyimbo, maombi na karatasi zingine zote kwa manufaa ya afya yao.

Aidha, mikutano yote na hafla za kanisa Katoliki pia zimesitishwa kwa kipindi sawia.

Kasisi Wainaina ametaka watu wote ambao walikuwa na mipango ya sherehe za harusi katika muda wa wiki nne zijazo kuzisitisha hadi pale hali ya kawaida itakaporejea.

Ibada za mazishi zitaendeshwa na makasisi wa kanisa japo kwa kundi la watu wasiozidi 10 pekee.

Mahubiri na maombi yatapatikana kwa njia ya mitandaoni kupitia tovuti ya kanisa na pia mitandao ya Facebook na Twitter.

Kasisi Wainaina ametaka waumini kutumia njia ya M-pesa na benki kutuma sadaka zao pamoja na fungu la kumi.