Kimataifa

CORONA: Hakuna Pasaka kanisani, misa zote zitapeperushwa mtandaoni

March 16th, 2020 1 min read

NA AFP

USIMAMIZI wa makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani yaliyoko jijini Vatican, umetangaza kwamba maadhimisho ya sikukuu ya Pasaka mwaka huu yatafanyika bila waumini kukongamana kutokana na tishio la virusi vya corona.

“Kutokana na janga la kiafya duniani linalotokana na virusi vya corona, sherehe za sikukuu ya Pasaka zitafanyika bila waumini,” ikasema taarifa kutoka Vatican.

Usimamizi huo una jukumu la kuratibisha shughuli za Papa Francis ikiwemo ziara yake katika mataifa mbalimbali duniani, watu wa kuhudhuria mikutano yake na mikutano kati yake na viongozi wa mataifa mbalimbali duniani.

“Hadi Aprili 12, Papa atakuwa akiongoza misa kupitia mtandaoni bila mtindo wa kawaida wa waumini kufika makanisani. Mahubiri yake pia yatakuwa yakipeperushwa kupitia mtandao wa Vatican,” ikaongeza taarifa hiyo.

Takwimu za hivi punde zinaonyesha kwamba watu 1,441 wamefariki nchini Italia baada ya kuambukizwa virusi vya corona huku wengine 21,000 wakiendelea kupokea matibabu.

Italia ndilo taifa ambalo limeathirika zaidi na corona barani Ulaya.