Habari

CORONA: Hali ya hatari nchini

March 22nd, 2020 1 min read

NA MWANDISHI WETU

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe Jumapili alitangaza kuwa watu wanane zaidi wanaugua  virusi hatari vya corona, baada ya kupimwa.

Wanane hao – Wakenya watano, Wafaransa wawili na raia moja wa Mexico – walithibishwa kuwa na virusi hivyo ambavyo kufikia jana vilikuwa vimeshika watu elfu 319 na zaidi ya elfu 13 kufariki kote duniani.

Vilevile wasafiri watakaoingia nchini kutoka taifa lolote la kigeni watatengwa katika taasisi za serikali kwa siku 14 kwa lazima na watagharimia kutengwa kwao.

Aidha watakaokosa kutii agizo la kujitenga kwa siku 14 watalazimishwa kufanya hivyo na watafunguliwa mashtaka mahakamani.

Wakenya walioko katika mataifa ya nje, pia wametakiwa kujitenga na kufuata kanuni za nchi hizo za kigeni.

Wakihutubu, kwenye kikao hicho, Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani Karanja Kibicho na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai walitoa kauli kali jinsi raia watakavyotakikana kutii maagizo yaliyotolewa.

Bw Kibicho aliamrisha utawala wa mkoa kuhakisha agizo la kufungwa kwa ibada zote msikitini na makanisani haikiukwi na yeyote na watakaokosa kutii wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Bw Mutyambai kwa upande wake alisema polisi watakuwa macho kuhakikisha kwamba mabaa yote yamefungwa na wahudumu wote katika sekta ya uchukuzi wanatii agizo la serikali la kubeba abiria wachache.

“Leseni za vyama vya wamiliki wa magari ambao watakaidi agizo la serikali zitafutiliwa mbali,” akasema Bw Mutyambai.